Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Tanzania inahitaji zaidi ujenzi wa hoja za maendeleo kupitia majadiliano ya kidemokrasia na utekelezaji wa mipango ya maendeleo, badala ya maandamano na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jun 13,2026,jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amesema CCM itaendelea kusimamia na kuimarisha siasa za maendeleo zinazolenga moja kwa moja kutatua changamoto za wananchi na kuboresha maisha yao.
Amesema chama hicho kinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa vitendo kupitia ziara mbalimbali za viongozi wake nchini, ambapo hukutana na wananchi katika mikutano ya hadhara na majukwaa tofauti kwa lengo la kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa kushirikiana na Serikali.
Kihongosi ameongeza kuwa CCM inaelewa vipaumbele vya wananchi ambavyo ni pamoja na huduma bora za afya, maji safi na salama, elimu bora, miundombinu imara na huduma nyingine muhimu za kijamii, hivyo Serikali inayoongozwa na CCM imeendelea kuelekeza nguvu katika sekta hizo ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati.
Kuhusu hali ya kisiasa nchini, amesema CCM imepokea taarifa mbalimbali zinazohusiana na madai ya kuwepo kwa mikutano ya siri inayodaiwa kufanywa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kwa lengo la kuhamasisha maandamano na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Amesema kutokana na hali hiyo, CCM inatoa wito kwa Watanzania wote kutoruhusu kutumika kwao katika ajenda zinazoweza kuleta vurugu, maandamano au uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa Tanzania imejengwa katika misingi ya utulivu, mshikamano na umoja wa kitaifa.
“Tunatoa rai kwa wazalendo wote na wapenda maendeleo kutoshabikia maandamano na vurugu kwa namna yoyote ile. Tanzania imejengwa katika misingi ya amani, mshikamano na utulivu, na tunapaswa kuilinda misingi hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.
Aidha, Kihongosi amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kuchochea migawanyiko na vurugu, hali ambayo imeendelea kuwa tishio kwa mshikamano wa taifa, huku akisisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuendelea kudumisha umoja bila kujali tofauti za kisiasa, kidini, kikabila au kieneo.
Ameeleza kuwa mara nyingi athari za maandamano huwakumba zaidi wananchi wa kawaida wakiwemo wafanyabiashara wadogo, wafanyakazi na vijana, huku familia za viongozi wa kisiasa zikiathirika kwa kiwango kidogo au kutoguswa moja kwa moja.
Amesema kutokana na hali hiyo, Tanzania inapaswa kuendelea kujenga hoja kupitia majadiliano ya kidemokrasia badala ya migogoro au uharibifu wa mali na maisha ya wananchi.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha umoja wa kitaifa na kutoruhusu kugawanywa kwa misingi ya dini, kabila, eneo au itikadi za kisiasa, akisisitiza kuwa nguvu ya taifa ipo katika mshikamano wake.
Pia ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuwa macho na kutekeleza wajibu wake wa kulinda amani na usalama wa raia na mali zao, huku akiwahimiza wananchi kushirikiana navyo kwa kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani.
Akizungumzia Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Kihongosi amesema bajeti hiyo imeonesha hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarika kwa uwezo wa taifa kujitegemea.
Ameipongeza Serikali pamoja na Bunge kwa kazi kubwa ya kuandaa na kupitisha bajeti hiyo, akisema itaendelea kuchochea maendeleo ya taifa, kuboresha huduma za kijamii na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Comments
Post a Comment