Serikali imesema Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 itaweka msingi imara wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku ikilenga kuharakisha ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuboresha ustawi wa wananchi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema bajeti hiyo ni ya kihistoria kwa kuwa ndiyo ya kwanza kutekeleza kwa vitendo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Juni 10, 2026, kabla ya kuwasilisha rasmi bajeti hiyo bungeni, Waziri Omar amesema Serikali inatarajia kutumia Shilingi trilioni 62.3 katika mwaka wa fedha 2026/27, ambapo sehemu kubwa itaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma muhimu za kijamii.
“Bajeti hii inakuja katika kipindi muhimu ambapo Taifa limeanza safari ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Dhamira yetu ni kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa jumuishi, endelevu na wenye manufaa kwa wananchi wote,” amesema Waziri Omar.
Ametaja maeneo yatakayopewa kipaumbele kuwa ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), uboreshaji wa miundombinu ya barabara, upanuzi wa huduma za maji na nishati, pamoja na uwekezaji katika elimu, afya na maendeleo ya ujuzi.
Kwa upande wa mapato, Serikali inalenga kukusanya Shilingi trilioni 46.8 kutoka vyanzo vya ndani, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea katika kugharamia shughuli zake za maendeleo.
Waziri Omar pia alisema utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2025/26 umeendelea kuonyesha mafanikio kutokana na ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya ndani, hali iliyowezesha Serikali kufikia malengo mbalimbali ya maendeleo.
Kuhusu maboresho ya kodi, ada na tozo, alisema Serikali ilipokea mapendekezo 727 kutoka kwa wadau mbalimbali, ambapo 125 yalipitishwa moja kwa moja na 121 kufanyiwa maboresho kabla ya kukubaliwa.
“Lengo la maboresho haya ni kukuza uchumi, kuvutia uwekezaji, kuongeza wigo wa walipa kodi na kuifanya mifumo ya kodi kuwa rafiki zaidi kwa wananchi,” amesisitiza.
Aidha, amewahimiza Watanzania kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati, huku akiwataka kufuatilia kwa karibu hotuba ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 itakayowasilishwa bungeni Juni 11, 2026 ili kuelewa vipaumbele na mwelekeo wa maendeleo ya Taifa katika mwaka mpya wa fedha.


Comments
Post a Comment