📍Dodoma
Tume ya Madini imesema kuanzishwa kwa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini kumeongeza uwazi katika biashara ya madini na kusaidia kudhibiti utoroshaji wa rasilimali hiyo, hatua iliyochangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali.
Akizungumza leo katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Afisa wa Tume ya Madini kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini, Ibrahim Akyoo, amesema mfumo huo umewezesha wachimbaji na wafanyabiashara kuuza madini kupitia njia rasmi na hivyo kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo.
Amesema kwa sasa nchini kuna masoko ya madini 44 na vituo vya ununuzi wa madini 120 vinavyorahisisha biashara ya madini na kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki yatokanayo na rasilimali hizo.
Akyoo amesema miongoni mwa majukumu ya Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini ni kusimamia biashara ya madini nchini, kuhakikisha ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo unaongezeka, kudhibiti utoroshaji wa madini, kufanya ukaguzi wa fedha na kodi pamoja na kutoa huduma za kimaabara kwa wadau wa sekta hiyo.
Amesema kupitia maonesho hayo, Tume ya Madini inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya madini, zikiwemo biashara ya madini, uchimbaji, uongezaji thamani, utoaji wa huduma na shughuli nyingine katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Amesema hatua hizo zinaendelea kuifanya sekta ya madini kuwa miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.








Comments
Post a Comment