WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka viongozi nchini wawaelimishe wananchi umuhimu wa kuandikishana mikataba wanapopeana ardhi badala ya kuendelea kufanya hivyo kwa kuaminiana.
"Viongozi mliopo hapa waambieni wananchi hivi sasa masuala ya ardhi wasifanye kwa kuaminiana, wawe wanaandikishana kwa mikataba na tena katika ofisi za kijiji ili watambulike," amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Juni 7, 2026) wakati akizungumza na viongozi wa kada mbalimbali wa mkoa wa Iringa katika kikao cha majumuisho ya ziara zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, mjini Iringa.
"Ninawasihi wananchi tusiogope kurasmisha mambo yetu kwa sababu uaminifu unaenda unapungua. Tunaporasmisha, tunaepusha migogoro siku za usoni," amesisitiza.
Waziri Mkuu ametoa rai hiyo kutokana na wingi wa kero zinazojitokeza kwenye mikutano aliyoishaifanya na hasa kwenye sekta ya ardhi.
Amewataka viongozi wanapotaka kufanya uendelezaji wowote nao pia wahakikishe wanawapa wananchi husika mikataba ili kulinda haki yao.
"Tusichukue maeneo ya watu bila kuwalipa fidia. Kama kuna uendelezaji ni lazima kuwe na mikataba rasmi. Wananchi wa eneo husika wapewe barua za kuonesha utwaaji huo wakati wakisubiri fedha za fidia zipatikane. Liwe ni eneo limetengwa kwa uwekezaji, ujenzi wa barabara au shule, watu wapewe barua. Ardhi ni jambo rasmi ndiyo sababu presha ya matumizi inazidi kuongezeka."
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wanapokuwa kazini wavae vitambulisho vyenye majina yao ili iwe rahisi kuwatambua.
"Watumishi wa umma wavae vitambulisho ili tuwatambue kwa urahisi wale wanaotukwamisha. Tusirasimishe uozo kwenye ofisi zetu. Zipo ofisi utakuta wanaofanya kazi ni asilimia 20 lakini wanaoenda kazini ni asilimia 80. Twendeni tuchape kazi na kila mmoja amsimamie aliyekabidhiwa chini yake."
Ametumia fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Heri James, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, Daudi Yassin na viongozi wote kwa kusimamia vizuri shughuli za maendeleo ya mkoa wao.
"Hongereni sana kwa sababu mkoa wenu umetulia. Nimepita majimbo yote saba sijakutana na ghasia za kugombea nafasi za uongozi. Katika maeneo yote, watu wenu wanaongelea masuala ya maendeleo."
Amesema wakati wa ziara zake, kuna baadhi ya hoja ziliibuliwa na wananchi lakini viongozi wa wilaya na mkoa walikuwa tayari wameshachukua hatua na hata ilipobidi mtu asafirishwe hawakusita kufanya hivyo.
Waziri Mkuu alianza ziara za mkoa wa Iringa Mei 2, mwaka huu kwa kutembelea Halmashauri zote tano na majimbo yote saba kila alipopata nafasi za mwisho wa wiki na leo amefanya majumuisho ya ziara zake.





Comments
Post a Comment