Na Gideon Gregory - Dodoma
Katika kipindi ambacho dunia inaendelea kukabiliwa na ongezeko la joto, uchafuzi wa mazingira mjadala kuhusu mazingira haupo tena kwenye uhifadhi pekee bali umehamia kwenye namna ambavyo mataifa yanajenga maendeleo yanayodumu.
Takwimu za Umoja wa Mataifa za miaka ya hivi karibuni zinaonyesha kuwa shinikizo la mazingira linaongezeka kila mwaka na kufanya hatua za sasa kuwa msingi wa maisha ya vizazi vijavyo.
Ni katika muktadha huo ambapo maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu kwa Tanzania yamekuja na ujumbe wa “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania” kauli inayobeba zaidi ya kampeni ya kupanda miti ili kurejesha uoto wa asili.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyila Jijini Dodoma Mei 5,2026 Makamu wa Rais Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi anabainisha kuwa mazingira yanamchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi.
"Pale ambapo mazingira yametunzwa vyema basi uchumi na ustawi wa maisha ya watu pia huimarika, aidha mazingira ni muhimu katika kuhimili ongezeko la watu duniani madhalani kwa Tanzania inakadiliwa kuwa na watu zaidi ya milioni 67 ambapo ifikapo mwaka 2050 idadi inakadiliwa kufikia zaidi ya watu milioni 118,"anasema.
Dkt. Nchimbi analitaja ongezeko hilo kubwa la watu kuhitaji uwepo wa rasilimali nyingi muhimu zinazotegemea mazingira kama vile maji, chakula, ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo, makazi, nishati na mfumo wa huduma za jamii, hivyo kwa kutambua umuhimu huo dira ya mwaka 2050 imejumuisha suala la mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kama sehemu ya maendeleo ya kuelekea uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya tani milioni 400 za plastiki huzalishwa duniani kila mwaka, huku karibu nusu yake ikitengenezwa kwa matumizi ya muda mfupi pekee na takribani asilimia 10 tu ndiyo hurejelewa (recycled).
Kati hizo tani milioni 19 hadi 23 za taka za plastiki huingia kwenye mifumo ya maji kila mwaka, na bila hatua za haraka kuchukuliwa kiwango hicho kinaweza kuongezeka kwa karibu asilimia 50 ifikapo mwaka 2040.
Hatua ambayo Dkt. Nchimbi anayataja maadhimisho hayo kama jukwaa muhimu la kitaifa na kimataifa la kukumbushia wajibu wa kuunganisha nguvu za pamoja katika jitihada za kuhifadhi mazingira na kuhakikisha matumizi sahihi dhidi ya rasilimali nyingi ambazo nchi imejaliwa ikiwemo kutoa elimu juu ya uhifadhi wa mazingira.
Kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Mataifa, uchafuzi wa plastiki leo haupo baharini pekee bali unaonekana kwenye udongo, maji na hata kupitia chembe ndogo za plastiki kwenye mazingira ya binadamu. Hii ndiyo sababu juhudi za mazingira sasa zinahusishwa moja kwa moja na afya, uchumi na ubora wa maisha.
Katika maadhimisho ya mwaka huu, mjadala wa kukijanisha Tanzania umeibuka kama zaidi ya kampeni ya kupanda miti, dhana yake ni kujenga mfumo wa maisha unaounganisha maendeleo, uchumi na uhifadhi wa mazingira kwa wakati mmoja.
Safari ya Tanzania ya kuelekea mwaka 2050 haitapimwa kwa ahadi zitakazotolewa leo pekee, bali kwa maamuzi yatakayofanywa, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mha. Hamad Masauni amesema kwasasa wameandaa mpango wa usimamizi wa mazingira kuelekea dira 2050 utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano.
"Mpango huu unalenga kuchochea matokeo makubwa ya kurejesha uoto wa asili, kuimarisha ustawi wa mfumo wa ikolojia pamoja na kutoa huduma za kiikolojia ambazo ni msingi muhimu za uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi hatua ambazo wanaamini zitachangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha malengo ya dira ifikapo 2050 ambayo yanalenga kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 barani Afrika zenye ustawi wa mazingira na ustahimilivu mkubwa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,"anasema.
Aidha, Mha. Masauni anasema kupitia mpango huo Serikali inatarajia kufanikisha malengo makuu mbalimbali ikiwemo kuhamasisha upandaji miti na utunzaji endelevu wa miti milioni 2 kila mwaka lakini kurejesha hekta milioni 5 za ardhi na misitu ambayo imeharibiwa na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Katika Siku hii ya Mazingira Duniani, ishara za tahadhari ziko kila mahali, Miaka kumi na moja iliyopita imekuwa miaka kumi na moja yenye joto la juu zaidi kuwahi kurekodiwa, hatua ambayo wadau wa mazingira wanaitaja kama funzo la kuhakikisha mazingira yanaendelea kutunzwa.
Wanaeleza kuwa dunia kwasasa inaelekea kuzidi kwa muda kiwango cha nyuzi joto 1.5 ambapo kila sehemu ya ongezeko uleta madhara makubwa zaidi hasa kwa watu walio katika mazingira hatarishi zaidi.
"Jukumu letu ni kuhakikisha kuzidi huko kunakuwa kidogo iwezekanavyo na kwa muda mfupi na usalama mkubwa iwezekanavyo na kisha kupunguza haraka sana viwango vya joto, hilo linamaanisha kupunguza kwa kiasi kikubwa sana cha utoaji wa gesi chafuzi, kuharakisha mpito wa haki kutoka kwa matumizi ya nishati ya mafuta yasiyosafi kwenda kwenye nishati jadidifu ambayo ndiyo njia pekee endelevu ya kupunguza gharama na kuhakikisha usalama wa kweli wa nishati"wanasema.
Pia, wanaeleza kuwa ukanda wa Afrika Mashariki ndio ambao unaathirika zaidi na kuongezeka kwa joto tangu miaka ya 1960 mpaka sasa ambapo joto limekuwa likiongezeka kwa 0.7% mpaka 100.1% juu zaidi ya kiwango cha wastani wa kiwango cha dunia ambacho ni 0.1 mpaka 0.5 huku maeneo kama ya Kaskazini mwa Uganda na Kenya yakitajwa kuwa na joto la juu zaidi ambalo limepelekea maafa makubwa kwa watu wa maeneo hayo.
Mafanikio ya taifa la kijani hayatapimwa kwa idadi ya miche iliyopandwa, bali kwa uwezo wa wananchi kubadili matumizi ya kila siku kuanzia usimamizi wa taka, matumizi ya plastiki, uhifadhi wa vyanzo vya maji hadi upangaji wa makazi.
Hapa ndipo nafasi ya mwananchi wa kawaida inaanzia na kwa kijana anayechagua kutumia tena badala ya kutupa, kwa mfanyabiashara anayepunguza taka na kwa familia inayotunza matumizi ya maji hapo ndipo sera inaanza kuonekana kwenye uhalisia.
Tanzania inapozungumzia mwaka 2050, huenda swali lisiwe tumepanda miti mingapi bali ni tulijenga utamaduni wa kuishi kwa namna gani kuhakikisha mazingira yanalindwa, hivyo kukijanisha Tanzania si tukio la Juni 5 ila ni maamuzi ya kila siku inayofuata.



Comments
Post a Comment