Serikali imeendelea kuimarisha juhudi za kuboresha ubora wa elimu nchini kwa kuhamasisha ubunifu na umahiri wa walimu, ambapo walimu 3,153 wamejisajili kushiriki Shindano la Taifa la Stadi za Ufundishaji la mwaka 2026, linalolenga kuibua mbinu bunifu za ufundishaji na kujifunzia ili kuongeza matokeo bora ya elimu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuelekea hafla ya utoaji wa tuzo kwa washindi wa mashindano hayo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Afidhi Ameir, amesema shindano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mageuzi ya sekta ya elimu pamoja na Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa madarasa ya chini.
Amesema serikali inalichukulia shindano hilo kama jukwaa muhimu la kuwapa walimu nafasi ya kuonesha uwezo wao, kubadilishana uzoefu na kuibua mbinu mpya zinazoweza kuimarisha ufundishaji darasani.
"Shindano hili linatoa fursa kwa walimu kuonesha umahiri wao, kubadilishana uzoefu na kuibua mbinu bunifu zinazoweza kusaidia kuongeza ubora wa elimu na matokeo ya ujifunzaji kwa wanafunzi," amesema Ameir.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, kati ya walimu 3,153 waliojisajili kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa National Teaching Skills Competition System (TSCS), walimu 1,263 walikamilisha vigezo vyote kwa kuwasilisha video za ufundishaji pamoja na maandalio ya masomo kwa ajili ya tathmini.
Mashindano ya mwaka huu yanahusisha maeneo saba ya ushindani ambayo ni Kusoma kwa Darasa la Awali, Kiingereza kwa Darasa la Kwanza, Ufaraguzi wa Zana kwa Darasa la Pili, pamoja na masomo ya Fizikia, Hisabati, Business Studies na Computer Science kwa walimu wa shule za sekondari.
Ameeleza kuwa maeneo hayo yamechaguliwa kutokana na mchango wake katika kuimarisha stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), umahiri wa lugha ya Kiingereza, ujasiriamali na stadi za karne ya 21 zinazohitajika katika dunia ya sasa.
Aidha, amewahimiza walimu kote nchini kufuatilia mashindano hayo na kutumia mbinu zitakazooneshwa na washiriki bora ili kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji katika shule zao.
Mashindano hayo pia yanaunga mkono utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu uliozinduliwa na Samia Suluhu Hassan Januari 29, 2026, ukiwa na lengo la kuhakikisha kila mwanafunzi anapata stadi za msingi kwa kiwango kinachostahili.
Hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi itafanyika Juni 6, 2026 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Riziki Shemdoe.
Washindi wa nafasi ya kwanza katika kila eneo la ushindani watapata zawadi ya Shilingi milioni 2.5, kompyuta mpakato, vyeti vya ushindi na pongezi, huku shule zao zikikabidhiwa projekta.
Vilevile, baadhi ya shule za washindi wa elimu ya awali na msingi zitapatiwa vibao vya kielektroniki 100 vyenye thamani ya Shilingi milioni tano kwa ajili ya kuimarisha ujifunzaji wa kidijitali.
"Mwalimu mbunifu ni nguzo ya elimu bora; elimu bora ndiyo msingi wa taifa imara."
Kaulimbiu ya mwaka huu ni: "UFUNDISHAJI BORA, TAIFA IMARA."





Comments
Post a Comment