Na Mwandishi wetu Jovina Massano.
Uimarishaji uhifadhi unazidi kuboreshwa na Serikali ya awamu ya sita kwa kuweza kuanzisha maduka maalum ya kuuza nyara na kuweka historia mpya tangu Uhuru.
Uanzishwaji huo umechukuliwa mara baada ya Machifu kutoka makabila mbalimbali nchini kuiomba Serikali kuwezesha upatikanaji wa nyara kwa makundi yanayohitaji kuzitumia katika mila na desturi.
Maombi hayo yaliwasilishwa kwa Mh.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza wakati wa tamasha la Bulabo ambalo hufanyika kila Mwaka linalokutanisha Viongozi wa mila na desturi kwa maana ya machifu kutoka mikoa mbalimbali.
Katika tamasha hilo waliweza kumsimika Mh.Rais wa awamu ya sita kuwa Chifu mkuu na mmiliki wa mila na desturi zilizo njema huku wakimpa jina la Chifu Hangaya.
Chifu Hangaya hakusita kuchukua hatua madhubuti kwa kuanzisha maduka hayo kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) katika mikoa ya Mwanza na Arusha.
Umuhimu wa maduka haya yatawezesha usimamizi mzuri wa nyara na kuwasaidia wahitaji,waganga wa tiba asili na mbadala wakiwemo manju wa ngoma kuzipata kwa urahisi.
Mhifadhi wa wanyamapori kutoka TAWA Bw. Omary Mhando amesema uwepo wa Maduka hayo ni sehemu mojawapo ya kurasimisha nyara kwa utaratibu maalum kwa wahitaji.
Ameongeza kuwa Chifu Hangaya kwa usikivu na hekima aliyojaliwa ya kuzingatia na kutambua umuhimu wa mila na desturi hapa nchini ameweka utaratibu utakaoondoa adha na adhabu zilizokuwa zikiwakumba watumiaji wa nyara ambao hawakuwa na vibali maalum vya umiliki.
Mhando amewashauri wahitaji kutumia fursa za uwepo wa maduka hayo kuweza kufika na kupata umiliki halali wenye kuleta amani kwa mtumiaji wote na wahitaji hupewa leseni na vibali vya umiliki.
Pia amewakumbusha utaratibu wa kufuata pindi mtu anapohitaji kumiliki nyara kulingana na aina ya nyara unazohitaji ambapo kutakuwepo na ujazaji fomu maalum ya maombi,uthibitisho wa uraia kwa maana ya vitambulisho,picha ndogo 2 (passport size),barua ya mapendekezo kutoka kwa afisa Mtendaji wa Kijiji au kata wa eneo analofanyia shughuli zake,awe amesajiliwa na kupewa leseni na mamlaka husika na awe hajatiwa hatiani.
Baada ya kukamilisha hatua hizo Mkurugenzi atapokea za maombi kwa ajili ya kuhakiki ikiwa mtuma amekidhi vigezo na kuwa na sifa atapatiwa namba ya malipo Kisha kupewa stakabadhi ya malipo usajili,leseni,Cheti na Kisha kupewa nyara.
Aidha uhamishaji wa umiliki nyara kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine itamlazimu mmiliki wa awali kuandika na kuomba kuhamisha umiliki wa nyara kwenda kwa mtu mwingine.
Endapo maombi yakikubaliwa mwombaji atapewa bili na namba ya malipo ili kuweza kulipa tozo husika na baada ya kukamilisha malipo mwombaji atakabidhiwa stakabadhi ya malipo ndipo uhamisho wa hati hiyo utaganyika kwa wote kisha kusaini nyuma kwenye hati miliki na mwisho afisa anaesimamia uhamisho huo naye atasaini.
Ikumbukwe kuwa nyara ni mnyamapori alie hai au kufa lakini pia sehemu ya mnyama huyo ikiwemo pembe,jino,mifupa,kucha,kwato,ngozi,nyama, mafuta,damu,manyoya,yai, pamoja na nyara zinazotengenezwa.
Hata hivyo nyara hutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo za mila na tamaduni,mafunzo,utafiti na mapambo.
Nae Katibu Mtendaji wa Umoja wa Machifu Tanzania Mtemi Harun Mkomangwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambae pia ndie Chifu mkuu kwa kutimiza maombi yao ya uwepo wa maduka maalum kwa ajili ununuaji wa nyara hizo.
Lakini pia amewahamasisha waganga wa tiba asili na mbadala kutembelea na kununua nyara hizo.






Comments
Post a Comment