Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali imeendelea kuimarisha tahadhari na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa Ebola ili kuzuia hatari ya ugonjwa huo kuingia na kusambaa nchini.
Akijibu maswali ya Papo kwa Papo Bungeni jijini Dodoma leo Juni 4, 2026, Dkt. Mwigulu alisema Tanzania inaendelea kuwa na mahusiano ya karibu na mataifa jirani kupitia shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni, hali inayochochea mwingiliano wa watu kuvuka mipaka na hivyo kuhitaji umakini mkubwa katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kinga ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia majukwaa tofauti, kuhamasisha wananchi kuzingatia tahadhari za kiafya na kuimarisha ufuatiliaji katika maeneo ya mipakani na sehemu nyingine muhimu.
“Tanzania si kisiwa. Kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika mapambano dhidi ya Ebola kwa kuzingatia tahadhari na kutoa taarifa mapema pale anapoona dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa huo,” amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Waziri Mkuu amewahimiza wananchi kuendelea kuelimishana kuhusu njia za kujikinga na Ebola na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini dalili zinazotia shaka, ili hatua za haraka zichukuliwe na kuzuia maambukizi kusambaa.
Pia amesisitiza umuhimu wa wasafiri wanaoingia nchini kushirikiana na wataalamu wa afya kwa kufanyiwa uchunguzi na kutoa taarifa sahihi kuhusu hali zao za kiafya bila kuficha dalili zozote.
Kauli hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kulinda afya za Watanzania kupitia hatua madhubuti za kinga, uelimishaji wa umma na ushirikiano wa wananchi katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko, huku ikisisitiza kuwa tahadhari za mapema ni silaha muhimu katika kuzuia kuenea kwa Ebola.







Comments
Post a Comment