*Kutoka: Dawati la Habari Polisi Mwanza*
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limemfikisha mahakamani mshtakiwa wa tatu, Benson John (19), mlinzi (Baunsa), mkazi wa Nyakabungo, Kata ya Isamilo wilayani Nyamagana na kumuunganisha katika kesi ya mauaji ya mkazi wa Mwanza, Mzafuru Faisal Yunusu.
Mzafuru anadaiwa kuuawa kwa kipigo katika baa ya Las Vegas iliyopo eneo la Kona ya Bwiru, mtaa wa Nyamanoro, wilaya ya Ilemela baada ya kushindwa kulipa bili ya shilingi 8000.
Hatua hiyo imekuja leo Juni 3, 2026, baada ya Wakili wa Serikali, Mwanahawa Changale, kuwasilisha ombi mahakamani hapo la kutaka hati mpya ya mashtaka inayomwongeza mtuhumiwa huyo ipokelewe chini ya kifungu cha 251 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Kufuatia marekebisho hayo ya hati ya mashtaka katika shauri la jinai namba 10492 la mwaka 2026, idadi ya washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo sasa imefikia watatu, ambao ni Yohana Paul Peter (22) ambaye ni mlinzi wa eneo hilo (Baunsa), Hamis Juma Mussa (27) mfanyakazi wa usafi, pamoja na Benson John (19), mlinzi (Baunsa) aliyeunganishwa leo.
Washtakiwa wote watatu wamepandishwa kizimbani na kusomewa shtaka hilo la mauaji mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Mhe. Juma Opudo kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Christian Mwalimu, ambaye ndiye msikilizaji wa shauri hilo.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mwanahawa Changale, akisaidiana na Clara Muhando, aliieleza mahakama kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo mnamo Februri 5, 2026 wakiwa katika baa hiyo ya Las Vegas ambapo wanadaiwa kumshambulia na kumuua Mzafuru Faisal Yunusu kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Hata hivyo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Wilaya haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza mashauri ya mauaji, ambayo kisheria ngazi hiyo ya mahakama inayatumia kwa ajili ya kutajwa tu kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Hakimu Opudo amefafanua kuwa kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, washtakiwa hawatatakiwa kukiri au kukataa tuhuma hizo, na kuongeza kuwa kosa la mauaji halina dhamana kisheria, hivyo wataendelea kubaki mahabusu hadi pale upelelezi utakapokamilika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 17,2026 saa nne asubuhi baada ya taratibu za kisheria za kumuunganisha mtuhumiwa huyo mpya kukamilika leo mahakamani na washtakiwa wote watatu wamerejeshwa rumande kusubiri tarehe inayofuata ya kutajwa kwa shauri hilo.





Comments
Post a Comment