Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, amewataka vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujipanga kikamilifu ili kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali, ikiwemo fedha za Shilingi bilioni 200 zilizotengwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jun 3,2026 katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma Dkt. Mahera amesema Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kuinua uchumi wa wananchi kupitia mikopo na miradi ya maendeleo, huku Halmashauri ya Butiama ikiendelea kusimamia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalumu, ambapo asilimia 4 hutolewa kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.
"Vijana wetu wanapaswa kujipanga vizuri ili waweze kunufaika na fedha hizi zinazolenga kuwawezesha kiuchumi na kuboresha maisha yao," amesema Dkt. Mahera.
Mbali na mikopo hiyo, amesema wizara mbalimbali zimeendelea kuonesha dhamira ya kushirikiana na wananchi wa Butiama katika kutatua changamoto zinazowakabili ambapo ametaja Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuwa imeahidi kutembelea jimbo hilo ili kutathmini maeneo yenye changamoto ya huduma za simu na kubaini njia bora za kuboresha mawasiliano.
Katika sekta ya utalii, Dkt. Mahera amesema jitihada zinaendelea kufanyika kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Butiama, hususan kutokana na historia yake ya kuwa nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Aidha, amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa miradi muhimu ya barabara ikiwemo barabara ya Nyankanga–Rung'abure kuelekea Serengeti, ambapo upembuzi yakinifu umekamilika na hatua zinazofuata ni kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
Pia ameieleza kuwa barabara ya Busegwe–Kitaramanga yenye urefu wa kilomita 38.5, ambayo ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Butiama, imeendelea kupewa kipaumbele na Serikali na inatarajiwa kuanza hatua za maandalizi katika mwaka wa fedha 2026/27.
"Kuna mambo mengi mazuri yanaendelea kufanyika katika Jimbo la Butiama, na tunaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na fursa za maendeleo ya kiuchumi," amesema Dkt. Mahera.


Comments
Post a Comment