Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera , amesema Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa Fedha 2026/27 pamoja na fedha zinazotolewa kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI zimeendelea kuonesha mwelekeo chanya wa Serikali katika kuimarisha huduma za afya ngazi ya msingi, huku Wilaya ya Butiama ikitarajiwa kunufaika na miradi mikubwa ya miundombinu ya afya.
Akizungumza leo Jun 3,2026 Katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma, Dkt. Mahera amesema uwekezaji huo utaongeza upatikanaji wa huduma bora, karibu na wananchi, na kupunguza changamoto ya umbali wa kufuata huduma za afya.
Amesema katika mgawanyo wa fedha hizo, Hospitali ya Wilaya ya Butiama imepangiwa Shilingi milioni 500 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa majengo, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa wengi zaidi na kuboresha utoaji wa huduma za kitaalamu.
Aidha, Serikali imetenga Shilingi milioni 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vituo viwili vya afya, ambapo Kituo cha Afya Butuguli na Kituo cha Afya Buhemba kila kimoja kitapokea Shilingi milioni 150 ili kukamilisha miundombinu na kuanza kutoa huduma kikamilifu.
Katika ngazi ya zahanati, Mahera amesema Zahanati ya Kijiji cha Nyanza imepangiwa Shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wake, pamoja na Zahanati ya Nyakiswa (Kata ya Kianyari) ambayo nayo imepangiwa Shilingi milioni 80, hatua inayolenga kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi wa vijijini.
Vilevile, kupitia Mradi wa TIMCHIP, Wilaya ya Butiama imepata Shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kirumi, mradi ambao unatarajiwa kuimarisha kwa kiasi kikubwa huduma za afya katika eneo hilo na kupunguza msongamano katika vituo vingine.
Mahera amesema kwa ujumla miradi hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya, hususan huduma za afya ya msingi ambazo zinagusa maisha ya wananchi wengi zaidi.
“Kwa upande wa sekta ya afya, bajeti ya Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI imegusa moja kwa moja huduma za afya ngazi ya msingi. Butiama tumepata miradi mikubwa ambayo itaimarisha miundombinu na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi wetu,” amesema Mahera.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi yote hiyo utaanza rasmi mwezi Julai mwaka huu na kuendelea hadi Julai mwaka ujao, huku akisisitiza kuwa uwekezaji huo ni hatua muhimu katika kuboresha ustawi wa wananchi wa Butiama na kuongeza ufanisi wa mfumo wa afya kwa ujumla.
“Hii ni zaidi ya ujenzi wa majengo ni uwekezaji katika afya, maisha na maendeleo ya wananchi wa Butiama.”

Comments
Post a Comment