Tanzania na Msumbiji zimechukua hatua mpya ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya ulinzi na usalama baada ya mawaziri wa ulinzi wa nchi hizo mbili kukutana na kusaini makubaliano mbalimbali ya kimkakati yatakayowanufaisha pande zote.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam wakati Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania, Rhimo Nyansaho, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji, Cristóvão Chume, katika Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyopo Upanga.
Mazungumzo hayo yalijikita katika namna ya kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji, hususan katika masuala ya ulinzi, usalama na maslahi ya pamoja ya mataifa hayo jirani.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa sekta ya ulinzi kutoka nchi zote mbili, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Faraji Kasidi Mnyepe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jacob John Mkunda, pamoja na maafisa wengine waandamizi.
Ziara ya Waziri Chume nchini Tanzania imelenga kuimarisha zaidi uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Mozambique, huku makubaliano yaliyosainiwa yakitarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wenye tija katika kulinda amani, usalama na utulivu wa mataifa hayo na ukanda kwa ujumla.




Comments
Post a Comment