Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum, ameibuka na kulaani vikali kauli za baadhi ya maseneta wa Bunge la Marekani waliodai kuwa Tanzania si salama na kwamba kuna ubaguzi wa kidini dhidi ya baadhi ya waumini nchini.
Akizungumza leo Mei 26, 2026 jijini Dodoma katika mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na JMAT, Sheikh Alhad amesema madai hayo ni ya uongo, uchochezi na hayana uhalisia wowote ndani ya Tanzania.
JMAT ni jumuiya inayounganisha madhehebu mbalimbali ya dini za Kiislamu, Kikristo pamoja na dini nyingine nchini kwa lengo la kuimarisha amani, maridhiano na mshikamano wa Taifa.
“Uwepo wetu hapa leo ni ushahidi wa wazi kwamba Tanzania hakuna udini. Tunaitaka Serikali ya Marekani iwakemee maseneta hao mara moja na kueleza wazi kuwa kauli hizo ni maoni yao binafsi,” amesema Sheikh Alhad.
Amesema Watanzania wamejenga maisha ya upendo, umoja na kuheshimiana kwa miaka mingi bila kujali tofauti za dini, jambo ambalo limeendelea kuifanya Tanzania kuwa mfano wa amani barani Afrika.
“Kauli hizi zimetuumiza sana kama Watanzania, kwa sababu umoja tulionao ni mkubwa. Hata viongozi wa dini tuliopo hapa ni mfano wa undugu wa damu kati ya Waislamu na Wakristo,” amesema.
Sheikh Alhad Amesisitiza kuwa viongozi wa dini nchini wamekuwa wakishirikiana kwa karibu katika kulinda amani na mshikamano wa Taifa, hivyo jitihada zozote za kuleta uchonganishi wa kidini hazitafanikiwa.
“Maseneta hao wamechelewa. Tanzania inaongozwa kwa misingi ya sheria, kanuni na Katiba. Uchochezi wa kidini au kisiasa hatutaukubali kamwe,” ameongeza.
Aidha, amesema Watanzania wanaendelea kuungana pamoja na Serikali pamoja na viongozi wa dini katika kupinga siasa za chuki, udini na vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Comments
Post a Comment