Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Askofu Israel Maasa, amesema Tanzania imeendelea kudumisha amani, mshikamano na uhuru wa kuabudu kwa zaidi ya nusu karne, hali iliyowafanya wananchi wa dini mbalimbali kuishi kwa upendo na ushirikiano mkubwa.
Askofu Maasa amesema Watanzania wamekuwa wakishirikiana katika shughuli za maendeleo, kufanya biashara pamoja, kujenga urafiki na hata kuoana kati ya familia za dini tofauti bila kuwepo migogoro ya kidini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 26, 2026 jijini Dodoma, amesema hali hiyo imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye utulivu mkubwa barani Afrika.
“Tuhuma na shutuma dhidi ya uwepo wa ubaguzi wa kidini nchini Tanzania zimetusikitisha, kutukasirisha na kutufedhehesha,” amesema Askofu Maasa.
Amesema hata raia wa Marekani wanaoishi Tanzania ni mashahidi wa namna uhuru wa kuabudu unavyoheshimiwa na kuimarika nchini.
“Hatutaki kuamini kwamba Marekani, taifa ambalo tuliungana nalo katika majonzi wakati wa mashambulizi ya kigaidi kwenye Ubalozi wake jijini Dar es Salaam mwaka 1998, leo linaweza kuhusishwa na hoja za kupotosha kuhusu Tanzania,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, JMAT imelitaka Bunge la Marekani kupinga hoja zinazodai kuwepo kwa ubaguzi wa kidini nchini Tanzania, ikieleza kuwa madai hayo hayana ukweli na yanaweza kuchochea migawanyiko isiyokuwepo.
“Hoja hizi zina lengo la kupandikiza chuki na kuharibu mshikamano wa Taifa letu. Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na umoja wa kitaifa,” mesisitiza.
Katika hatua nyingine, JMAT imeitaka Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya mapitio ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani ili kulinda maslahi ya Taifa na kuzuia uchonganishi wa kidini.
Aidha, jumuiya hiyo imempongeza Rais Dkt.Samia kwa hatua mbalimbali alizochukua kushughulikia changamoto zilizojitokeza mwaka 2025, ikiwemo kuunda Tume ya Uchunguzi na Tume ya Jinai kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji, haki, maridhiano na kufungua njia ya kupatikana kwa Katiba Mpya aliyoiahidi.

Comments
Post a Comment