Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb) tarehe 09 April, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mheshimiwa Guy Kabombo Muadiamvita aliyefanya ziara ya kikazi nchini Tanzania. Mazungumzo hayo ya Kikazi baina ya Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yalifanyika katika Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo jijini Dodoma, yalilenga kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu na kihistoria baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika Diplomasia ya Ulinzi.
Katika kikao hicho, Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Rhimo Nyansaho amemhakikishia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kongo,utayari wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ulinzi na JKT, kushirikiana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika nyanja mbalimbali za Ulinzi, hususani katika Ubadilishanaji wa wataalamu, Mafunzo, pamoja na ushirikiano dhidi ya changamoto za kiusalama kama, Uhalifu wa mtandaoni na vita dhidi ya ugaidi.
Dkt Rhimo Nyansaho amemueleza Mgeni wake Naibu Waziri Mkuu wa Kongo Mhe, Guy Kabombo kuwa, ziara yake nchini Tanzania, ni ushahidi wa uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili huku ikionyesha umuhimu mkubwa katika kuendelea kudumisha na kuimarisha maelewano, ushirikiano na urafiki kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuongeza kuwa kwa miaka mingi kumekuwa na majadiliano ya wazi yenye nia ya kujenga na kuweka misingi ya ushirikiano madhubuti kati ya Tanzania na Kongo.
“Nina Imani kuwa kupitia ushirikiano na uhusiano wetu sio kwamba tutakabiliana na changamoto zinazotukabili kwa pamoja, pia tutanufaika na fursa zilizopo mbele yetu ili kuchochea ukuaji na ustawi wa pamoja”, alisema Dkt. Rhimo Nyansaho.
Naye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe Guy Kabombo Muadiamvita akizungumza katika kikao hicho amesema ziara yake nchini ina lengo la kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Tanzania na kusema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo inayoongozwa na Rais Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo inaiona Tanzania kama mshirika mkubwa wa kimkakati katika ushirikiano wa maendeleo.
Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuongeza kuwa ni matarajio yake kuwa kupitia majadiliano mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanyika yatasaidia nchi yake kuibua kwa undani maeneo muhimu ambayo Serikali ya Tanzania inahitaji kuendelea kushirikiana na nchi yake.
Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimekuwa zikishirikiana katika nyanja za Kilimo, Biashara na uwekezaji, pamoja na masuala ya Ulinzi na Usalama.
Kikao hicho katika ya Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Rhimo Nyansaho na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe Guy Kabombo Muadiamvita, kilihudhuriwa pia na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini Tanzania, Balozi Jean Pierre Massala, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na JKT, Dkt Faraji Kasidi Mnyepe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe Meja Jenerali Lukwikila Metikwiza Marcel na maafisa waandamizi toka Wizara ya Ulinzi na JKT ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,pamoja maafisa waandamizi toka wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania.







