SERIKALI imetangaza kufuta leseni 40 za uchimbaji wa madini kwa wamiliki walioshindwa kutekeleza masharti ya kisheria, ikisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha sekta ya madini inachangia kikamilifu maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Hatua ya kufuta leseni 40 inaashiria msimamo thabiti wa Serikali wa kuendeleza Sekta ya Madini dhidi ya uzembe na vitendo visivyo halali, huku ikifungua ukurasa mpya wa uwajibikaji na ushindani wa haki katika matumizi ya rasilimali za Taifa.
Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema tayari walishatoa hati za makosa kwa wahusika, lakini bado hawakukidhi matakwa ya sheria, hivyo kulazimika kuchukua hatua ya mwisho ya kufuta leseni hizo kwa mujibu wa sheria.
“Kuna wamiliki wa leseni ambao hawaziendelezi kwa wakati, wanahodhi maeneo, hawalipi ada stahiki, na hawatekelezi wajibu wa ushirikishwaji wa Watanzania pamoja na wajibu kwa jamii,” amesema
Aidha, amesema kuwa Kuna baadhi ya wamiliki hao wanashindwa hata kuwasilisha vielelezo vinavyoonesha matumizi ya fedha katika shughuli za uendelezaji wa leseni zao, hali inayodhoofisha uwajibikaji katika sekta hiyo muhimu ya uchumi.
Katika kudhibiti hali hiyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua za haraka kila panapojitokeza matukio ya mlipuko wa madini (gold rush), kwa lengo la kulinda usalama wa wananchi na mali zao pamoja na mazingira.
“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna migogoro, tunalinda mazingira na kudhibiti hatari za kiafya zinazoweza kujitokeza katika maeneo ya msongamano mkubwa,” amefafanua
"Maeneo ya “gold rush” yamekuwa yakihusisha mkusanyiko mkubwa wa watu katika mazingira yasiyo rasmi, hali inayoongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa ya mlipuko. Kutokana na hilo, Serikali imekuwa ikiratibu huduma za afya za dharura, kuhakikisha usafi wa mazingira, upatikanaji wa maji safi, pamoja na kutoa elimu ya kinga kwa wachimbaji na wadau". Ameongeza
Kadhalika, amesema Baada ya hali kutulia, Serikali hufanya tathmini ya kina ya maeneo hayo, na pale inapobainika kuwa hayana leseni halali, huchukua hatua za urasimishaji ili kuweka mfumo rasmi wa uchimbaji unaofuata sheria.
Amesema pamoja na juhudi hizo, Wizara imeeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa vitendo vya uvamizi wa maeneo yenye leseni halali, vinavyofanywa na baadhi ya wachimbaji wadogo wasio waaminifu.
“Tabia ya kuvamia maeneo yenye leseni halali kwa kisingizio cha ‘gold rush’ ni marufuku. Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika,” amesisitiza
Ameongeza kuwa vitendo hivyo vinasababisha migogoro, hasara kwa wawekezaji halali na kuvuruga utaratibu mzima wa usimamizi wa sekta ya madini nchini.
Aidha, Mheshimiwa Mavunde,amekemea tabia inayoongezeka ya baadhi ya wachimbaji wadogo kuvamia maeneo yenye leseni halali, akieleza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaokiuka sheria.
“Tutaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wa ndani na nje wanaolenga uwekezaji wenye tija kwa maendeleo ya Taifa letu,”. Amesema
Sambamba na hayo, Mheshimiwa Mavunde amesema Vitendo vya kuhodhi leseni vimekuwa chanzo kikubwa cha migogoro na kuchochea uchimbaji holela, hali inayohatarisha usalama wa wananchi, mazingira na mapato ya Serikali.
Serikali inawakumbusha kuwa maendeleo endelevu ya sekta ya madini yanategemea nidhamu, uzingatiaji wa sheria na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wawekezaji na wananchi.



