Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetoa taarifa rasmi kwa umma likikanusha picha mjongeo (video) inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuonyesha kichwa cha treni ya SGR kikiwa kinatoa mlio usio wa kawaida.
TRC imethibitisha kuwa taarifa hizo ni za uzushi na zinalenga kupotosha umma, kwani baada ya ufuatiliaji wa kina, imebainika kuwa hakuna tukio kama hilo lililotokea katika mifumo yao ya uendeshaji.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo tarehe 20 Aprili 2026 na Kitengo cha Uhusiano, Shirika la Reli Tanzania (TRC) Shirika hilo limehakikishia umma kuwa treni zote za mwendokasi (SGR) zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na ziko katika hali salama kabisa.
Aidha, hakuna hitilafu yoyote ya kiufundi iliyoripotiwa na wataalamu wanaoendesha na kusimamia mitambo hiyo kama inavyodaiwa kwenye video hiyo ya uzushi.
"TRC inasisitiza kuwa usalama wa abiria na mali zao ni kipaumbele cha juu. Mifumo yote ya uendeshaji hukaguliwa mara kwa mara na wataalamu wetu ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ubora wa kimataifa,"* ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Shirika limetoa wito kwa wananchi kupuuza video hiyo na kutoendelea kuisambaza kwani haina ukweli wowote. TRC imewataka Watanzania kutumia vyanzo rasmi vya habari vya Shirika hilo ili kupata taarifa sahihi na za uhakika kuhusu huduma za reli nchini.
TRC imeendelea kuwahakikishia Watanzania kuwa huduma za treni ya kisasa ya SGR ni salama, za uhakika, na zinaendelea kuboreshwa kila siku ili kukidhi mahitaji ya usafiri kwa wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.
