Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited inayomilikiwa na mfanyabiashara Rostam Aziz, imeingia makubaliano ya kununua sehemu ya hisa katika biashara ya gesi ya Orca Energy Group Inc. nchini Tanzania, hatua inayotajwa kuwa ya kihistoria katika sekta ya nishati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 13, 2026, Taifa Gas itanunua asilimia 49 ya hisa za kampuni ya PAE PanAfrican Energy Corporation (PAEM), huku kampuni ya Amber Energy Investment L.L.C-FZ ikichukua asilimia 51 iliyobaki.
Makubaliano hayo yanahusisha uuzaji wa asilimia 100 ya biashara ya Orca nchini Tanzania, ikiwemo haki zake zote katika mradi wa gesi wa Songo Songo, ambao ni mhimili muhimu wa uzalishaji wa gesi kwa matumizi ya umeme na viwanda.
Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya mabadiliko makubwa ya umiliki katika sekta ya gesi, ambapo wawekezaji wa ndani wanaanza kuchukua nafasi kubwa zaidi katika rasilimali za kimkakati.
Akizungumzia maendeleo hayo, Rostam alisema mpango huo umechukua muda mrefu kuandaliwa na unalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na rasilimali zake za asili.

