Taifa Gasi yaunga mkono jitihada za serikali matumizi ya Nishati safi

GEORGE MARATO TV
0

 





Na MASHAKA MHANDO, Lushoto


IMEELEZWA kuwa zaidi ya Watanzania 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya nishati zisizo safi kama kuni na mkaa, hali inayolifanya Taifa kuingia katika msiba mzito wa nguvu kazi kila kukicha.


Kufuatia takwimu hizo za kutisha, Kampuni ya Taifa Gas, ambayo ni kinara wa nishati safi nchini, imetangaza kuongeza uwekezaji wake na kasi ya usambazaji wa gesi ili kuunga mkono juhudi za dhati za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anayepigania matumizi ya nishati mbadala barani Afrika na duniani kote.


Akizungumza Leo wilayani Lushoto, Meneja wa Masoko wa Taifa Gas, Oscar Shelukindo, amebainisha kuwa kampuni hiyo sasa inashikilia asilimia 51 ya soko la gesi nchini, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa katika miundombinu inayolenga kumkomoa mwanamke wa Kitanzania na mazingira kwa ujumla.


"Mafanikio haya ya kumiliki asilimia 51 ya soko yametokana na dhamira yetu ya kuunga mkono juhudi za Taifa. Tunataka kuwabadilisha Watanzania kutoka kwenye nishati zinazoua (kuni na mkaa) na kuwahamasisha kutumia gesi iliyo salama, safi na yenye gharama nafuu kwa afya na mazingira," alisema Shelukindo.


Elimu na Mikakati ya Kufika Kijijini


Shelukindo aliongeza kuwa Taifa Gas imeamua kupeleka huduma hiyo hadi ngazi ya chini kwa kutoa mitungi ya kilo 6 na 15 kwa bei ya ushindani, sambamba na kutoa elimu ya matumizi sahihi. 


Katika hatua nyingine ya kimkakati, Taifa Gas kwa kushirikiana na Benki ya NMB wanatarajia kushiriki katika Tamasha la Kijiji Day, ambapo watatoa huduma za nishati safi na elimu kwa jamii, hatua inayolenga kuhakikisha elimu ya nishati mbadala inafika hadi vitongoji vya ndani.


Juhudi hizi za Taifa Gas zinaonekana kuwa chachu ya mabadiliko chanya yanayoendana na dira ya Rais Samia ya kulinda mazingira na kuimarisha afya za Watanzania, huku ikipunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya vifo vinavyotokana na moshi wa kuni majumbani.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top