Serikali inapenda kutoa ufafanuzi kwa umma kufuatia taarifa potofu iliyotolewa na
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuhusu uteuzi wa Mbunge uliofanywa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 02 Aprili 2026 chini ya Ibara ya
66(1)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni sahihi kuwa kabla ya uteuzi huo, Mheshimwa Angela Kizigha alikuwa Mbunge wa
Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Hata hivyo, kwa mujibu wa Ibara ya 51(3)(c) ya Mkataba wa Kuanzishwa kwa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, Mbunge wa EALA hukoma kuwa Mbunge endapo atateuliwa
kuwa Mbunge wa Bunge la Nchi Mwanachama.
Kutokana na masharti hayo, ubunge wa EALA kwa Mheshimiwa Angela Kizigha na
Waheshimiwa Dkt. Ngwaru Maghembe na James Milya ulikoma baada ya
kuteuliwa/kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Aidha, Ibara ya 50 ikisomwa pamoja na Ibara ya 52 ya Mkataba inatoa mamlaka kwa
Bunge la Nchi Mwanachama kujaza nafasi zilizo wazi katika Bunge la Jumuiya ya
Afrika Mashariki kulingana ratiba zake kama zitakavyopangwa kwa mujibu wa
taratibu husika.
Hivyo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litajaza nafasi tatu (3)
zilizoachwa wazi, kama itakavyolezwa katika ratiba ya shughuli za Bunge. Aidha,
inapaswa kufahamika kuwa mchakato wa kujaza nafasi hizo unapaswa kuanzia
katika vyama vya siasa ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 50(1) ya Mkataba wa
Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa msingi huo, Serikali inasisitiza kuwa hakuna mgongano wowote kati ya uteuzi
uliofanywa chini ya Katiba na masharti ya Mkataba wa Kuanzishwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
