Na Dawati la Habari Polisi; Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewatoa hofu wakazi wa Wilaya ya Ukerewe kufuatia kuibuka kwa viashiria vya uvunjifu wa amani baada ya kutokea kwa tukio la kijana mmoja, Leonard Mganga (44), mkazi wa Kitongoji cha Kabo, Kijiji cha Nampisi na kujeruhi waumini wawili wa kanisa katoliki.
Mtuhumiwa huyo aliingia Kanisa la Bikira Maria Mama wa Tumaini Jema, Parokia ya Kagunguli, Jimbo Katoliki la Bunda kupitia mlango mdogo kulia mwa jengo hilo na kuwashambulia kwa panga waumini wawili baada ya kutolewa nje, hali iliyozua taharuki kubwa wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya Dominika ya Pasaka.
Tukio hilo lilitokea tarehe 5 Aprili, 2026, majira ya saa 1:30 asubuhi, ambapo kijana huyo aliingia kanisani akiwa amebeba mfuko uliokuwa na panga alilolitumia kuwashambulia waumini hao. Mtuhumiwa huyo alipoteza maisha kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa na waumini pamoja na wananchi wenye hasira waliokuwepo eneo la tukio.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Kagunguli, viongozi wa dini, na watumishi wa serikali mnamo Aprili 10, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa, amesema Wilaya ya Ukerewe imekuwa na mfululizo wa matukio yenye sura mbaya kwa jamii. Alibainisha kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha hofu kwa wananchi wa Ukerewe na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla.
Kamanda Mutafungwa alitaja baadhi ya matukio hayo kuwa ni pamoja na harakati za watu wanaojiita 'Kamchape', ambao hujidai kuwa na uwezo wa kuondoa uchawi na kuwahadaa wananchi ili kuwatapeli fedha na mali zao.
Tukio jingine ni la binti wa miaka 18, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kornel Magembe, aliyeripotiwa kukamatwa na mamba Machi 2 mwaka huu alfajiri akiwa anaoga kwenye fukwe za ziwa victoria kwa maandalizi ya kwenda shuleni, kisha kuonekana akiwa hai eneo lilelile baada ya siku saba, jambo lililozua taharuki. Tukio la tatu ni hilo la Leonard Mganga (44) kuvamia kanisa na kujeruhi watu kabla ya kuuawa na umati.
“Haya yote niliyoyataja yameshughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Sasa, kwa sababu leo ninyi ni wawakilishi wa wenzenu wengi walioko Kagunguli na Ukerewe kwa ujumla, kama kuna changamoto yoyote ya kiusalama, twambieni,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Kushamiri kwa matukio hayo kulimlazimu Kamanda wa Polisi kufika kuzungumza na wananchi sambamba na kutoa elimu ya usalama na Polisi Jamii. Aidha, alitoa maelekezo kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), SSP Elija Matiko, pamoja na Polisi Kata kuhakikisha wanaifikia jamii kwa kutoa elimu itakayosaidia kukomesha vitendo vya namna hiyo.
“Tunaruhusiwa kufanya ukamataji salama, lakini hatuna mamlaka ya kuwahukumu watu. Mtu anapofanya kosa la kihalifu, wajibu wetu kama wakazi wa Kagunguli ni kumkamata kwa usalama na kumkabidhi kwenye vyombo vya dola ili haki itendeke. Haturuhusiwi kabisa kujichukulia sheria mkononi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Richard Mganga, mkazi wa Kata ya Kagunguli, amesema elimu iliyotolewa na Kamanda Mutafungwa ni ya msingi na ina umuhimu mkubwa kwani imewabadilisha na kuwafundisha namna ya kuripoti na kufichua viashiria vya uvunjifu wa amani.
Naye Yasinta Mgoma, mkazi wa kata hiyo, alilaani kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi kilichosababisha kifo cha kijana huyo aliyevamia kanisa wakati ibada ikiendelea.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa ametembelea Kanisa la Bikira Maria Mama wa Tumaini Jema, Parokia ya Kagunguli, Jimbo la Bunda pamoja na familia ya marehe Leonard kupata maelezo ya kina kuhusu tukio lililotokea sikukuu ya Pasaka.








