Naibu Spika wa Bunge la Tanzania na Mhe. Daniel Baran Sillo (Mb) amewakaribisha rasmi wawakilishi wa mabunge yote wanachama wa IPU kuhudhuria Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) utakaofanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 5 hadi 9 Oktoba, 2026
Akizungumza katika sherehe za kufunga Mkutano wa 152 wa IPU jijini Istanbul, Uturuki, Mhe. Sillo ameishukuru Serikali na Bunge la Uturuki chini ya Spika *Mhe. Numan KurtulmuÅŸ* kwa ukarimu na maandalizi mazuri yaliyofanikisha mkutano huo.
Mhe. Sillo amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Bunge imejipanga kikamilifu kupokea wageni hao.
Ameeleza kuwa Tanzania ni nchi ya amani tangu uhuru 1961, yenye makabila zaidi ya 120 yanayoishi kwa umoja chini ya mwavuli wa lugha ya Kiswahili.
“Tuna methali isemayo ‘Mgeni aje Mwenyeji apone’. Kwa mantiki hiyo, tumedhamiria kuhakikisha wajumbe wote wanapata VISA-FREE na VISA-ON-ARRIVAL,” amesema Mhe. Sillo.
Amefafanua kuwa mkutano huo utafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), kilichopo katikati ya jiji maarufu kama "Geneva ya Afrika", chini ya Mlima Meru.
Amesema hoteli za malazi zimeshatambuliwa na wajumbe wanaombwa kufanya booking mapema.
Sambamba na hayo, Mhe. Sillo amewaalika wajumbe kuchangamkia fursa ya kutembelea vivutio vya utalii vya kiwango cha dunia vilivyopo Tanzania vikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kreta ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Visiwa vya Zanzibar.
Wakati akihitimisha hotuba yake, Naibu Spika aliomba hadhira ya mkutano huo kumsikiliza Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu kwenye video maalum iliyoandaliwa kuonesha utayari wa Tanzania kuandaa mkutano wa 153, fursa za uwekezaji zilizopo na utalii.

















