Balozi Yakubu akutana na wadau wa Tanzania France Chamber of Commerce kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi

GEORGE MARATO TV
0


Balozi mteule wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, leo amekutana na viongozi na wanachama wa Tanzania France Chamber of Commerce katika kikao cha kujadili namna ya kuimarisha mahusiano ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Ufaransa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake ya kuanza rasmi majukumu yake jijini Paris.

Katika kikao hicho, Balozi Yakubu alipata fursa ya kupewa tathmini ya kina kuhusu uwekezaji wa Ufaransa nchini Tanzania, ambapo imeelezwa kuwa uwekezaji wa kampuni za Kifaransa umefikia takriban dola za Marekani bilioni 1.3, huku baadhi ya kampuni hizo zikiwepo nchini kwa zaidi ya miaka 30.

Akizungumza katika mkutano huo, Balozi Yakubu alisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa karibu na sekta binafsi ya Ufaransa. Aliahidi kushirikiana kwa karibu na wadau hao ili kuongeza mtiririko wa biashara, kuvutia uwekezaji mpya, na kuitangaza Tanzania kama lango la biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Aidha, majadiliano yaligusa fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, nishati, miundombinu na viwanda, huku pande zote zikionesha nia ya dhati ya kuendeleza ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Balozi Yakubu pia alimshukuru Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Anne-Sophie Ave, kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha diplomasia ya umma na kukuza mahusiano ya kirafiki kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa upande wake, Rais wa Chamber, Christophe Darmoy, alieleza utayari wa sekta binafsi ya Ufaransa kuendelea kuwekeza nchini Tanzania na kushirikiana na Serikali katika miradi ya maendeleo.

Mkutano huo umeweka msingi imara wa kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Ufaransa, hususan katika kukuza biashara, uwekezaji na diplomasia ya kiuchumi.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top