SERIKALI imeendelea kusisitiza utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 inayotaka taasisi zote za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalum, yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, ikiwa ni mkakati wa kukuza uchumi jumuishi nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, wakati akiwasilisha mada kuhusu fursa za zabuni za umma kupitia Mfumo wa NeST, katika kongamano la kuadhimisha miaka 104 ya kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Kongamano hilo lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma na kufunguliwa Rasmi na Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Katika wasilisho lake, Bw. Simba alibainisha kuwa mfumo wa NeST umeboreshwa ili kurahisisha ushiriki wa makundi maalum katika zabuni za umma, huku akihimiza vijana kuchangamkia fursa hizo ili kujijengea uwezo wa kiuchumi.
“Sheria hii siyo tu mwongozo wa manunuzi, bali ni chombo muhimu cha kuwawezesha wananchi kiuchumi, hasa makundi maalumu ambayo kwa muda mrefu hayakupata fursa sawa,” imeeleza serikali.
Sambamba na hilo, PPRA iliweka kambi maalum katika kongamano hilo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu zabuni za umma pamoja na huduma ya usajili katika Mfumo wa NeST kwa wazabuni na makundi maalum.
Serikali pia imezitaka taasisi nunuzi kuhakikisha malipo kwa makundi hayo yanatolewa kwa wakati, hatua inayolenga kuimarisha biashara zao na kuwapa uwezo wa kukua kiuchumi.
Kwa mujibu wa serikali, wanufaika wa mpango huo ni pamoja na vijana kama nguvu kazi ya Taifa, wanawake wanaochangia ustawi wa familia, wazee wenye uzoefu mkubwa pamoja na watu wenye ulemavu wanaohitaji ushiriki jumuishi katika maendeleo.
“Lengo ni kuona hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika maendeleo. Kila kundi lina nafasi ya kushiriki na kunufaika na rasilimali za nchi,” serikali imesisitiza.
Katika kuimarisha utekelezaji wa mpango huo, halmashauri zote Tanzania Bara zimeelekezwa kusaidia makundi hayo kuunda vikundi, kuvisajili katika mfumo wa NeST na kukamilisha taratibu kupitia PPRA ili kushiriki kikamilifu katika zabuni za umma.
Ajenda ya kuyawezesha makundi Maalumu ni sehemu ya ujumbe maalumu katika mbio za Mwenge wa Uhuru Kwa mwaka huu 2026 ikiwa ni dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha makundi hayo yanainuliwa kiuchumi na hivyo kukuza ajira na kupambana na umasikini miongoni mwao.
Wananchi pia wamehimizwa kutafuta elimu zaidi kuhusu fursa hizo kupitia ofisi za PPRA, ofisi zake za kanda au tovuti rasmi ya taasisi hiyo.
Kwa upande wa Zanzibar, utekelezaji wa mpango huo unasimamiwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 2 ya mwaka 2025, huku serikali ikiendelea kukamilisha kanuni zake ili kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya kiuchumi.
“Kukamilika kwa kanuni hizi kutafungua milango mipya ya fursa kwa wananchi wa Zanzibar na kuongeza ushiriki wao katika uchumi,” imeeleza serikali.
Kwa ujumla, utekelezaji wa asilimia 30 ya zabuni za umma unaelezwa kuwa ni hatua muhimu ya serikali katika kukuza uchumi shirikishi, kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza fursa za kujiajiri kupitia zabuni za umma.












Comments
Post a Comment