Msimu wa tatu wa Bunge Marathon umezinduliwa leo februari 27, 2027 katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam ambapo mwaka huu mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Aprili 18 2026 Jijini Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa Maadalizi ya mbio hizo Mhe. Festo Sanga amesema mbio hizo ambazo zinaandaliwa kwa mara tatu, zinatarajiwa kuwakutanisha wanariadha zaidi ya 5,000 kutoka ndani na je ya Tanzania.
Amesema Lengo la kuendeleza mbio hizi ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuimarisha afya kupitia michezo.
Akizungumzia zawadi za washindi Mheshimiwa Sanga amesema zawadi katika msimu huu wa tatu zimeboreshwa zaidi ambapo kwenye nusu marathon yaani kilometa 21, mshindi wa kwanza atajinyakulia Milioni 6, mshindi wa pili atapata Milioni 3 na mshindi wa tatu akiambulia Milioni 1.5.
Kwa upande wa kilomita 10, mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi milioni 3, mshindi wa pili Shilingi milioni 2, na mshindi wa tatu atajinyakulia shilingi milioni moja, huku katika kilomita 5 mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 2, nafasi ya pili akipata milioni moja na mshindi wa tatu atapata shilingi laki tano.
Mhe. Sanga amesema dirisha la usajili wa mbio hizi limefunguliwa rasmi kupitia tovuti ya maalum ya Bunge Marathon www.marathon.bunge.go.tz ambapo ada ya ushiriki wa mbio hizo ni shilingi elfu arobaini (40,000/-) ambayo mshiriki atapatiwa Marathon Kit itakayojumuisha fulana, mfuko na namba ya kukimbilia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Silent Ocean Ndg Mohamed Soloka amesema Bunge Marathon imebeba agenda zao zote ambazo ni afya na michezo, ndio maana wakashawishika kudhamini mbio hizo.
“Tumevutiwa na lengo la mbio hizi ndio maana tumedhamini, tunaunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kutumia michezo kuimarisha afya za Watanzania, lakini pia kama ajira kwa maendeleo mapana ya taifa letu “ amesema Soloka.














