Pigo kwa Upinzani Kenya,Baada ya Mahakama Kuu Kuharamisha Kampeni za Mapema kabla IEBC Kupuliza Kipenga

GEORGE MARATO TV
0

 KAMPENI za mapema nje ya kipindi kilichotengewa shughuli hiyo ni kinyume cha sheria na kanuni hitajika kwa uchaguzi huru na haki, Mahakama Kuu ya Kenya imeamua.

Majaji Hedwig Ong’udi, Patricia Gichohi na Heston Nyaga walisema kuwa kampeni za mapema pia zinasababisha madhara mbalimbali kwa raia.

Majaji hao walisema kampeni zinazoendeshwa nje ya kipindi cha uchaguzi zinavuruga haki ambazo raia wanapasa kufurahia kwa mujibu wa katiba.

“Bila shaka kipindi cha uchaguzi hushuhudia taharuki za kisiasa, wasiwasi, kauli za kuleta migawanyiko hali inayorudisha nyuma shughuli pana za kiuchumi,” wakasema majaji hao, wakiongeza kuwa ipo haja kwa wanasiasa kukomesha kampeni na wajikite katika masuala ya maendeleo ili kuinua maisha ya raia.

Majaji Ong’udi, Gichohi na Nyaga walitoa uamuzi huo katika Kesi iliyowasilishwa na shirika la kutetea haki, Kituo cha Sheria, kabla ya uchaguzi wa mkuu wa 2022.

Kulingana na majaji hao, watu wakijikita katika kampeni za kisiasa, aghalabu, husahau majukumu na wajibu wao katika maisha yao ya kila siku.

“Kile ambacho wanasiasa hutoa kama zawadi kwa kuhudhuria mikutano yao haiwezi kufananishwa na mapato yao ya kila siku.

 Aidha, hongo wanazopokea huleta migawanyiko katika jamii huku zawadi hizo zikiwafanya watu kuzoea kuwategemea wanasiasa,” mahakama Kuu ilisema.

Majaji Ong’udi, Gichoji na Nyaga waliamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Kenya Dorcas Oduor kuchukua hatua ndani ya miezi 12 kwa kuanzisha sheria ya kudhibiti kampeni za kisiasa, zinazoendeshwa nje ya kipindi maalum cha uchaguzi.

Mahakama ilisema Mwanasheria Mkuu yuko na wajibu wa kuweka sheria hiyo akishirikiana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) “ili kuzuia kampeni za mapema”.

Kituo cha Sheria kilisema kuwa kampuni za mapema hutoa nafasi ya kutokea kwa fujo za kisiasa, matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi na ufujaji wa pesa za umma.

Sheria ya Uchaguzi, miongoni mwa masuala mengine, inaipa IEBC mamlaka ya kutenga kipindi cha kampeni na shughuli zingine za uchaguzi kama vile kura za mchujo kuteua wagombeaji wa nyadhifa mbalimbali. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top