Balozi Matinyi awasilisha Hati ya utambulisho kwa Mfalme wa Sweden

GEORGE MARATO TV
0

 

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, amewasilisha rasmi Hati za Utambulisho kwa Mfalme Carl XVI Gustaf, katika hafla maalum iliyofanyika tarehe 12 Juni, 2025, katika Kasri la Mfalme wa Sweden, jijini Stockholm. 

Baada ya mazungumzo mafupi kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufalme wa Uswidi, Mhe. Balozi Matinyi alisindikizwa kwa gwaride rasmi kuelekea kwenye Kasri la Kifalme na kuwasilisha hati hizo kwa Mfalme Carl XVI Gustaf, ikiwa ni ishara rasmi ya kuanza kazi yake kama mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden.

Katika mazungumzo yao mafupi, Mhe. Balozi Matinyi alimfikishia Mfalme Carl XVI Gustaf salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwake yeye binafsi pamoja na serikali na watu wa Uswidi.

Mhe. Balozi Matinyi alimwelezea pia Mfalme Carl XVI Gustaf dhamira ya Tanzania ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizi mbili na nia ya kukuza ushirikiano katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, hususani katika uwekezaji, biashara, utalii, elimu na mafunzo ya ufundi, afya, nishati, miundombinu, utunzaji mazingira, pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

Kwa upande wake, Mfalme Carl XVI Gustaf alituma salamu za undugu na urafiki kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan; na kueleza kuwa nchi yake ya Uswidi itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa manufaa ya mataifa yote mawili, hususani katika kuendeleza sekta za viwanda, nishati, madini, utalii na elimu.

Itakumbukwa kuwa, Mhe. Matinyi aliteuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uswidi mnamo tarehe 25 Machi 2025, ambapo pia atakuwa na jukumu la kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Denmark, Finland, Iceland, Norway, Estonia, Latvia, Lithuania na Ukraine.


Stockholm, Sweden.

14 Juni, 2025.

Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi akiwa katika picha rasmi na Mfalme Carl XVI Gustaf wa Sweden mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mfalme tarehe 12 Juni, 2025, jijini Stockholm (Picha na Lisa Raihle wa Ofisi ya Kasri la Mfalme wa Sweden).

Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa wa Kasri la Mfalme wa Sweden (wa pili kushoto na wa mwisho kulia) na Ofisa Msindikizaji wa Mabalozi (kushoto kwake) mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mfalme Carl XVI Gustaf wa Sweden tarehe 12 Juni, 2025, jijini Stockholm. Balozi Matinyi aliambatana na maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden: Ofisa Mambo ya Nje Mwandamizi Tunsume Mwangolombe (wa kwanza kushoto); Ofisa Mambo ya Nje Mkuu Malik Hassan (wa nne kutoka kulia); Ofisa Mambo ya Nje Mwandamizi Abel Maganya (wa tatu kutoka kulia) na Mwambata wa Utawala Yunge Massa (wa pili kutoka kulia). (Picha na Lisa Raihle Rehbäck wa Ofisi ya Kasri la Mfalme wa Sweden).

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top