Profesa Kithure Kindiki aapishwa kuwa Naibu rais wa kenya

GEORGE MARATO TV
0


Profesa Kithure Kindiki ameapishwa kuwa naibu rais wa Jamhuri ya kenya. 

Profesa Kindiki amechukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua aliyeondolewa ofisini na Bunge la kitaifa na Bunge la seneti baada ya kuhusishwa na tuhuma kadhaa zikiwemo za kuendeleza ukabila. 

Akizungumza Mara baada ya kula kiapo,Profesa Kindiki ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria za nchi pamoja na kumshauri vyema Rais wa taifa hilo Dkt.William Ruto. 


Profesa Kindiki ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa waziri wa usalama wa ndani na utawala wa Taifa na anakuwa Naibu rais wa 14 katika historia ya kenya na wa tatu chini ya katiba mpya ya mwaka 2010.


Kabla ya kuteuliwa waziri mwaka 2022 na Naibu rais mwaka 2024,Profesa Kithure Kindiki alihudumu kama seneta wa kaunti ya Tharaka Nithi kuanzia mwaka 2013 hadi 2022 ambapo katika kipindi hicho pia alihudumu kama Naibu Spika wa Bunge la Seneti pamoja na kiongozi wa wengi katika Seneti. 



Akiwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti, aliongoza ajenda ya kutunga sheria ya chama cha wengi katika Seneti.

Kindiki pia amefundisha sheria na kushikilia nyadhifa mbalimbali za utawala katika kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Moi na kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Nairobi.

 Alianza taaluma yake kama Mhadhiri Msaidizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Moi punde tu baada ya kuhitimu na shahada ya kwanza ya sheria.

Kisha alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kama Mhadhiri baada ya kuhitimu Shahada ya Uzamifu katika Sheria ya Kimataifa ambapo alipandishwa cheo haraka hadi Mkuu wa Idara ya Sheria ya Umma akiwa na umri wa miaka 33 na kisha kuwa Msimamizi Msaidizi akiwa na umri wa miaka 35.

Baadaye Kindiki alipandishwa cheo kuwa  Profesa Mwandamizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Ameandika machapisho thelathini na matano yakiwemo vitabu, sura za vitabu na makala katika majarida nchini na kimataifa.

Profesa Kindiki ana Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu cha Moi, Diploma ya Uzamili ya Sheria kutoka Shule ya Sheria ya Kenya, Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M), na Shahada ya Uzamifu (Ph.D.) katika sheria ya Kimataifa  kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini.

Aliwakilisha Rais Ruto katika kesi iliyomkabili katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top