Mtanda amebainisha hayo katika kongamano la viongozi wa dini mkoani mwanza lililolenga kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo utakaofanyika November 27 mwaka huu.
Mtanda ametumia kikao hicho kilichoshirikisha kamati ya amani ya viongozi wa dini kusisitiza kuwa Mambo ya kukimbia na masanduku ya kura yamepitwa na wakati.
"Uchaguzi wa serikali za mitaa ni mchakato, hatuna mpango wa kumzuia mgombea yeyote kuchukua fomu,kila aliyejiandilisha atapata fursa ya kupiga kura,kura zitahesabiwa kwa uwazi na kushuhudiwa na wakala wa kila mgombea na matokeo halali ndio yatatangazwa" Alisema Mtanda na kuongeza kuwa
"Kuhusu suala la amani,tumejiandaa kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unapita salama na hakuna anayeguswa kwa namna yeyote,wajibu wetu ni kukumbushana na kuhimizana suala amani ili wachache wenye nia ovu waache''.
Amesema serikali inatambua umuhimu wa demokrasia na kwamba upatikanaji wa viongozi wenye uhalali ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akitoa mada kwenye kikao hicho,Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la Kivulini Yassin Ally amewaasa viongozi wa dini kuhamasisha makundi yote ya kijamii kujitokeza kuchagua viongozi wanaowataka Katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Ally pia amehimiza umuhimu wa Jamii kuchagua viongozi wanawake pamoja na kudumisha amani kabla,wakati na baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
"Katika uchaguzi wagombea wanapaswa kutambua kuwa kuna kushinda na kushindwa,hivyo ni vyema watakaoshindwa wakubali matokeo ili kuepusha vurugu zinazoweza kujitokeza" alisema Ally
Viongozi wa dini mkoani mwanza wamekubaliana kuhamasisha Wananchi kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi wanaowataka Kama walivyojitokeza kwa wingi wakati wa zoezi la uandikishaji wapiga kura.
Mwenyekiti mwenza wa kamati ya amani ya viongozi wa dini Mkoa wa mwanza Sheikh Hassan Kabeke amewaasa Wananchi kudumisha amani wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
"Zipo taarifa wanawake hawakujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi,sasa twendeni tukawahamasishe wajitokeze kuchagua wagombea wanaowataka hususani wanawake ili kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye ngazi ya maamuzi" alisema sheikh Kabeke
Naye Mwenyekiti mwenza wa kamati ya amani ya viongozi wa dini mkoani mwanza Askofu Charles Sekelwa amehimiza Jamii kujiepusha kuchagua viongozi wala rushwa.










