Katibu muhtasi Maimuna Kanyamala atunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu nchini canada

GEORGE MARATO TV
0




Mwanzilishi wa shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la Kivulini Maimuna Kanyamala ametunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu(PHD)na Chuo kikuu cha Western cha nchini Canada.

Chuo hicho kimemtunuku shahada hiyo oktoba 16 mwaka huu baada ya kutambua mchango wake kwenye nyanja ya Maendeleo ya Jamii ikiwemo mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.


Kanyamala ambaye kitaaluma ni Katibu Muhtasi alilianzisha shirika la kivulini mwaka 1999 kufuatia kushamiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shirika la kivulini,shirika hilo linajivunia mafaniko mengi hususani kuwezesha Jamii kuvunja ukimya dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia. 

Hayo yamebainika wakati wa hafla ya kumpongeza Maimuna Kanyamala kwa kutunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu na chuo kikuu cha Western cha nchini Canada.









Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyoandaliwa na shirika la kivulini,Kanyamala amelipongeza shirika hilo kwa kuendeleza vyema ndoto zake za kuhakikisha Jamii inavunja ukimya dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

‘’Wakati tunaanza harakati zetu mwaka 1999,ukatili wa kijinsia ulikuwa umeshamiri sana kwenye Jamii zetu,watu walikuwa wanaona ukatili kama Jambo la kawaida tofauti na sasa ambapo Jamii inavunja ukimya kuhusu ukatili na serikali inachukua hatua za kisheria dhidi ya wanaojihusisha na vitendo hivyo’’alisema Kanyamala na kuongeza kuwa

‘’kivulini kwa kweli wanavuma sana,wakati nilipokuwepo mimi kama  mkurugenzi na mwanzilishi tulikuwa kwenye mikoa michache lakini sasa hivi kivulini iko kwenye mikoa mingi,mimi sikupata nafasi ya kufanya kazi moja kwa moja na waziri kwa kuja kwenye Jamii,lakini sasa tunaona viongozi mbalimbali hata waziri wa maendeleo ya Jamii,Jinsia,wanawake na Makundi Maalum Dokta Dorothy Gwajima siku za karibuni alikuja na kutembelea shughuli zinazofanywa na kivulini.

Amesema kuwa ufanisi wa shirika la kivulini umemjengea amani kuwa ameliacha shirika hilo kwenye mikono salama na kuwaasa wafanyakazi kudumisha ushirikiano miongoni mwao ili kuongeza tija zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Yasin Ally amesema mwanzilishi wa shirika hilo Maimuna Kanyamala anastahili tuzo hiyo kutokana na kutoa mchango mkubwa katika kumwezesha mwanamke kiuchumi na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wanawake.

‘’Baada ya kutambulika mchango wake kimataifa,Tuliona hatuna budi na sisi kumpongeza kwa dhati kwa sababu kazi ya kivulini ukiuliza hapa Tanzania,afrika na duniani inatambulika’’alisema Yaasin

Wakizungumza kwenye hafla hiyo,baadhi ya watu ambao maisha yao yameguswa na Kanyamala wakiwemo wahanga wa ukatili wa kijinsia wamesema kuwa harakati zake zimewawezesha kupiga hatua za kimaendeleo.

Wakati wa harakati zake,kanyamala amewajengea akinamama wengi wakiwemo wahanga wa ukatili wa kijinsia uwezo wa kujikwamua kiuchumi pamoja na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye chama pamoja na serikali.














 




 


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top