Na Emmanuel Chibasa
Katika mwalo
wa Kayenze ndogo, wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza, wavuvi na wafanyabiashara
wa dagaa sasa wanashuhudia mabadiliko makubwa kupitia teknolojia ya kisasa ya
nishati ya jua, inayotumika kukausha dagaa. Mradi huu, unaoendeshwa na kampuni
ya Millennium Engineers, umeleta matumaini mapya kwa sekta ya uvuvi kwa
kuwawezesha wavuvi kukausha dagaa kwa ubora unaokidhi viwango vya soko la ndani
na nje ya nchi.
Kwa Nini Teknolojia Hii ni Muhimu?
Teknolojia
mpya ya ukaushaji dagaa kwa kutumia mitambo ya nishati ya jua ni muhimu kutokana
na kutajwa kuwa suluhisho la kukabiliana na changamoto ya upotevu na uchakataji
wa dagaa zenye ubora na hivyo kuongeza tija kwa wavuvi na wachuuzi katika ziwa
victoria.
Wavuvi na
wafanyabiashara ya dagaa wanasema, Kabla ya mradi huo, wailikua wakianika
dagaa kwenye mchanga au kwenye vichanja vya miti kando ya ziwa Victoria na njia
hizi za jadi zilikuwa na changamoto kadhaa, zikiwemo kuathiri usafi wa dagaa,
kuvutia uchafu na wadudu, na kusababisha upotevu wa dagaa kutokana na hali ya
hewa isiyotabirika. Teknolojia ya nishati ya jua imebadilisha hali hiyo kwa
kuwezesha dagaa kukauka kwa usafi na haraka, na hivyo kuongeza thamani ya
bidhaa.
Agness Selestine ni mmoja wa wafanyabiashara wa dagaa, amesema ukaushaji kwa kutumia nishati ya jua umewapunguzia changamoto nyingi, hasa wakati wa mvua.
“Dagaa sasa
zinakauka haraka na zikiwa safi zaidi, tofauti na ilivyokuwa kwa kukausha
kwenye mchanga."
Naye Latifa Buchoji kwa upande wake anasema teknolojia hiyo mpya imewapa uhakika wa ubora wa dagaa, ambao unakubalika zaidi kwenye masoko hata ya nje hivyo ni mkombozi kwa biashara yao.
Madhara ya Kunianika Dagaa kwenye
Mchanga
Dagaa, ni
chakula maarufu duniani na wanatajwa
kuwa na faida nyingi katika mwili wa binadamu ikiwa ni pamoja na kuongeza faida kwa chakula cha usawa, kwa kuwa ni
chini ya mafuta yaliyojaa na kalori, lakini juu ya protini. Pia hutoa safu
nzuri ya vitamini na madini lakini wataalam wa lishe wanasema kuna madhara
kadhaa kwa binadamu endapo dagaa wataanikwa katika mchanga na sehemu isiyo
salama ambayo ni pamoja na;
Hatari ya Uchafuzi: Kuwaanika dagaa moja kwa
moja kwenye mchanga huwafanya wachafuke na kupata vumbi, bakteria, na uchafu
mwingine ambao unaweza kusababisha magonjwa ya njia ya chakula.
Vimelea vya Magonjwa: Mchanga una bakteria na vimelea vinavyoweza kusababisha maambukizi ya magonjwa kama vile kuhara, kipindupindu, na magonjwa mengine ya tumbo. Dagaa walioanikwa chini wanaweza kuwa na vimelea hawa hatari kwa afya.
Sumu na
Kemikali: Mchanga unaweza kuwa na sumu au kemikali kutoka kwenye mazingira
yanayozunguka, ambazo zinaweza kupenya kwenye dagaa. Hii inahatarisha afya kwa
muda mrefu iwapo dagaa walio na sumu hizi wataliwa mara kwa mara.
Ubora wa
Chini wa Lishe: Dagaa walioanikwa chini wanaweza kupoteza baadhi ya virutubisho
muhimu kutokana na kuathirika na vumbi na jua kali moja kwa moja, hivyo
kupunguza thamani ya lishe ya dagaa hao.
Harufu na Ladha Mbaya: Dagaa walioanikwa kwenye mchanga wanaweza kupata harufu na ladha ya vumbi, hali ambayo inawafanya wasiwe na ladha nzuri na kuvutia kwa walaji.
Jinsi Mradi Huu Unavyofanya Kazi
Kwa mujibu
wa mtaalamu wa nishati ya jua kutoka Millennium Engineers Mhandisi Wistone Nnko
anesema kabla ya kuanzisha mradi huo wafanya biashara na wavuvi walikua
wanaanika dagaa katika mchanga au katika vichanja na walikua wakitumia muda
mrefu katika kazi hiyo.
“Mradi wetu umekuja kuleta mapinduzi katika sekta ya uvuvi ziwa Victoria, ambapo wavuvi walikua wanakabiliwa na changamoto mbambali ikiwa ni pamoja nyenzo za uvuvi wakati wa usiku walikua wanatumia karabai ambazo sio rafiki kwa mazingira, lakini pia katika eneo la ukaushaji, ambapo walikua wanafanya kazi katika eneo ambalo sio salama na walikua wanatumia masaa nane hadi kumi kwa siku.
Tumeleta
teknolojia ya kisasa yanayotumia solar kukausha
dagaa, ambapo wakina mama baada ya kununua dagaa kwa wavuvi wanaleta hapa
kiwandani, wakileta tunazipima na kuzifanyia usafi kisha tunaanza na kuziweka
kwenye dryer ambayo inatumia masaa
matatu tu kukausha dagaa, mradi wetu umekuja kuongeza ubora wa mazao ambayo
yanatokana na dagaa na kufikia vigezo vya kimataifa ili watu wanaofanya kazi
kwenye hii sekta wanufaike na wanachokifanya” Amesema Mhandisi Wistone
Uwekezaji katika Taa za Sola kwa
Mavuno Bora
Mbali na
kukausha dagaa, mradi huu pia unalenga kuzalisha na kusambaza taa za sola zenye
mwanga wa kutosha kwa ajili ya shughuli za uvuvi. Taa hizi zinaweza kuchochea
mavuno bora kwa wavuvi wa dagaa na hivyo kusaidia kuboresha maisha yao.
Frank Faustine ni miongoni mwa wavuvi katika mwalo wa Kayenze Ndogo anasema tangu ameanza kutumia taa za solar amekua akivua dagaa wengi tofauti na alivyokua anatumia taa za karabai huku Mhandi Wistone akieleza jinsi teknolojia hiyo inavyoweza kusaidia wavuvi kutatua changamoto katika mialo tofauti ndani ya ziwa Victoria pamoja na kuwasaidia wafanyabiashara na wavuvi kutafuta masoko ya kimataifa ili waweze kupata faida zaidi.
"Taa za sola zinatoa mwanga wa kutosha unaosaidia kuvutia dagaa kwa wingi na kuokoa gharama za mafuta. Pia, zinatusaidia kuepuka uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya taa za karabai na betri za asidi, ambazo ni hatari kwa viumbe hai," amesema Frank.
Changamoto Zinazowakabili Wavuvi wa
Dagaa
Licha ya
mafanikio haya, bado kuna changamoto katika mialo mingine ya Ziwa Victoria kama
vile mwalo wa Busekera huko Musoma Vijijini na mwalo wa Makoko wilaya ya Musoma
Mjini. Katika maeneo haya, wavuvi bado hutegemea kukausha dagaa kwa njia za
jadi kwa kutumia mchanga au vichanja, hali inayosababisha hasara kubwa kutokana
na uchafu na hali ya hewa isiyotabirika. Ukosefu wa teknolojia hii husababisha
dagaa kushindwa kufikia viwango vya usafi vinavyohitajika kwenye soko la kimataifa,
hivyo kuathiri biashara.
Faida za Kuendeleza Teknolojia Katika
Maeneo Mengine
Ni dhahiri
kuwa uwekezaji katika teknolojia ya nishati ya jua unaweza kuboresha hali ya
mialo mingine kama Busekera wilaya ya musoma vijijini na Makoko uliopo katika
manispaa ya Musoma. Kwa kutumia teknolojia hii, wavuvi wataweza kuboresha ubora
wa bidhaa zao, kupunguza upotevu wa dagaa, na kuongeza thamani ya biashara zao,
hivyo kufikia masoko ya kitaifa na kimataifa kwa urahisi zaidi.
Wito kwa Serikali na Wadau wa
Maendeleo
Mafanikio ya
teknolojia hii yanaonyesha kuwa uwekezaji katika nishati safi na rafiki kwa
mazingira una umuhimu mkubwa katika sekta ya uvuvi. Mhandisi Wistone Nnko
anatoa wito kwa serikali kutoa ruzuku ili kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya
nishati ya umeme jua kwa gharama nafuu kwa
wavuvu na wafanyabiashara katika sekta ya uvuvi.
“Naamini kwamba serikali ina malengo mazuri sana kwa sasa na baadae, teknolojia hizi ambazo zinakuja kutatua changamoto katika sekta ya uvuvi naiomba serikali itoe ruzuku ili tunaponunua vifaa kutoka nje ya nchi visitozwe kodi pale bandarini kwa kufanya hivyo tutavipata kwa bei ambayo ni rafiki lakini pia sisi pia tutakapo vipeleka kwa walengwa wa mwisho pia watavipata kwa gharama ambayo ni nafuu.
Tunatoa mwito kwa makampuni, taasisi za maendeleo, na serikali kuwekeza katika miradi kama hii ili kuwasaidia wavuvi wa dagaa wa Ziwa Victoria kufaidika na rasilimali za ziwa kwa njia endelevu.
Aidha, Sekta
inatoa ajira kwa watanzania zaidi ya milioni 6.0 pamoja na ajira za moja kwa
moja kwa wavuvi 198,475 na wakuzaji viumbe maji 35,986. Uzalishaji uliofanywa
na waajiriwa hawa umewezesha familia
kupata kipato pamoja na kuongeza usalama wa chakula na lishe ambapo Sekta
huchangia 46 asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama. Pia,inakadiriwa
kwamba, kwa wastani, kila mtanzania anakula kiasi cha kilo 7.9 kwa mtu kwa
mwaka.






