Rhobi Samwelly Awataka Wanafunzi wa Kike Chief Ihunyo Sekondari Kujitambua

GEORGE MARATO TV
0

 


Na Fresha Kinasa.

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) Rhobi Samwelly   amewataka wanafunzi wa kike wanaosoma kidato cha tano na  kidato cha sita Katika Sekondari  ya Wasichana  ya  Chief Ihunyo iliyopo Wilayani Butiama Mkoani Mara kusoma kwa bidii, kujisimamia na  kujitambua ili  watimize ndoto zao. 

Rhobi ambaye  amekuwa akijishughulisha na kutetea haki za wanawake na watoto kupitia Shirika analoliongoza, ameyasema hayo Octoba 30, 2024,  wakati akizungumza na Wanafunzi hao (580) shuleni hapo.  Ambapo pia,  ametoa elimu ya madhara ya  ukatili wa Kijinsia. 

Rhobi amesema kuwa, Taifa na Jamii inahitaji Wasomi wenye ujuzi na utaalamu  watakaosaidia kuendelea kuleta mageuzi chanya katika nyanja mbalimbali. Hivyo  amewahimiza  kutumia fursa waliyonayo kwa sasa kusoma kwa bidii na kuweka nidhamu mbele  kufikia malengo yao kwa ufanisi.  

Ametolea mfano Taifa la Tanzania linaongozwa na Rais mwanamke Dkt.  Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kiongozi bora na mahiri kitaifa na kimataifa kutokana na kusoma kwa bidii na kujitambua hadi kufika alipo kwa sasa. Ambapo  amewasisitiza pia  kuwa na maono ya kuwa viongozi kwa siku za usoni na maandalizi yao yaanze wakati huu kwa kujitambua thamani yao kikamilifu. 

"Niwaombe mjitambue thamani yenu wakati huu mkiwa na nafasi ya kusoma,  someni kwa bidii na kusimama kwa ujasiri bila kukubali vishawishi. Ninyi ni Viongozi wa baadaye na pia ni msaada kwa Jamii na Taifa letu zingatieni masomo yenu na kuwa na malengo kila mmoja wenu."amesema Rhobi Samwelly.

Pia, Rhobi amewataka wanafunzi hao,  kuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu ya ukatili wa Kijinsia kwa wengine. Huku akiiomba Jamii kuwawezesha Watoto wa kike kwa kuwapa mahitaji yao ya msingi na kuweka mazingira wezeshi ya wao  kufikia  ndoto zao.  

Kwa upande wake Janeth Peter Mwanafunzi wa Kidato cha Sita shuleni hapo akizungumza kwa niaba ya wanafunzi hao, amemshukuru Rhobi Samwelly kwa kupata fursa ya kuzungumza nao na kuwatia moyo jambo ambalo amesema limewapa ari na molari ya kijituma ili watimize ndoto zao.  

Naye Madame Gisela Kimario amesema kuwa, hatua ya Rhobi  Samwelly kuwapa elimu ya ukatili wa Kijinsia na kujitambua itawasaidia wanafunzi hao kusimama katika malengo yao na kuwa na uchungu wa kufanya vizuri katika mitihani  na masomo yao.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top