Kiongozi wa Huduma ya Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni,Augustine Bilomo Maarufu kwa Jina la Mfalme Tengwa amekemea usaliti unaofanywa na baadhi ya viongozi dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jijini Mwanza,Mfalme Tengwa amesema kuwa Rais Samia anajengewa fitina na watu wenye nia mbaya kwa lengo la kuzorotesha utawala wake.
Amedai kuwa baadhi ya makundi ambayo yamekuwa yakimhujumu na kumchafua Rais Samia ni pamoja na baadhi ya viongozi na watumishi wa umma,wafanyabiashara,Viongozi wa madhehebu ya dini na watu wa kada mbalimbali.
‘’Tanzania ina wasaliti,wanamfanyia hila Rais Samia ili aonekane ndiye anayetuma watu kuteka na kuuwa watu wakati si kweli,Mi mungu amenambia huyu mama ni ishara madhubuti ya Taifa hili ila kuna vitengo mbalimbali vinavyofanya kazi kinyume na Rais kwa nia ya kutaka kuuharibu uongozi wake’’alisema Mfamle Tengwa na kuongeza kuwa
‘’Rais Samia ni kiongozi wa kwanza nchini kuruhusu kufanyika kwa maandamano ya amani,Marais waliomtangulia hakuna aliyeruhusu maandamano hata kama ni amani,Mi nawashangaa sana baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo vilipewa fursa ya kuandamana na kupewa ulinzi lakini bado vinamtukana Rais,huo ni usaliti mbaya sana katika taifa’’
Pamoja na usaliti na uchochezi unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watu dhidi ya Ras Samia,Mfalme Tengwa ameeleza matumaini yake kuwa Rais ataibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na Maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyopatikana katika utawala wake.
‘’Mimi nayaonya makundi yote ya watanzania yanayomhujumu Rais yakiwemo yale yanayoteka na kuuwawa watu,Mikakati yao inajulikana hivyo waache mara moja hujuma hizo vinginevyo mungu atawashushia kipigo ambacho hawatakisahau’’alisema Mfalme Tengwa.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu ujao,Mfalme Tengwa amewaasa wanasiasa kukubali matokeo ili kuepusha vurugu zinazoweza kujitokeza na kuhatarisha amani na utulivu uliopo.
Naye Nabii Alpha Kihamba wa Huduma ya Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni amewahimiza watanzania kudumisha amani na utulivu ili kuepusha vurugu zinazoweza kujitokeza kabla,wakati na baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika oktoba 27 mwaka huu.
Nabii Kihamba amesema kuwa hakuna mbadala wa amani hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuwa mzalendo kwa Taifa lake ikiwemo kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza kwenye mkutano huo,Kihamba pia amewaasa viongozi wa dini kuhubiri injili ya kweli ili kujenga taifa la watu wenye hofu ya mungu pamoja na kutosita kukemea maovu yanayotendeka kwenye Jamii ikiwemo ushoga na ulawiti.








