Mkuu wa shule ya sekondari Capri-Point Thomas Mboya amesema kuwa mazingira ya utoaji wa elimu yamekuwa rafiki baada ya kutatuliwa kwa changamoto zilizokuwa zinaikabili shule hiyo.
Uhaba wa vyumba vya madarasa ni miongoni mwa changamoto zilizotatuliwa kwa kuongezwa kwa vyumba 14 vya madarasa vikiwemo 12 vya ghorofa pamoja na vyumba viwili vya kawaida.
Shule hiyo pia imeondokana na uhaba wa na Dawati baada ya serikali kuipatia viti na meza 640.
Akizungumza katika mahafali ya 15 ya kidato cha nne,Mboya amesema kuwa vitabu vya masomo ya sayansi na Hisabati si tatizo baada ya kupokea vitabu 3,300 kutoka serikalini huku idadi ya walimu ikiongezeka Hadi kufikia walimu 32.
Aidha ameishukuru serikali kwa kuendelea na utekelezaji wa Sera ya elimu bila malipo ambayo imewapa watoto wengi wa kitanzania fursa ya kupata elimu.
Nao wahitimu kupitia risala iliyosomwa na Bora Shiranga wameishukuru serikali kwa kumaliza kabisa tatizo sugu la viti na meza pamoja na kuondoa upungufu wa vitabu vya kiada vya masomo ya sayansi.
Kuondolewa kwa uhaba wa vitabu vya kiada kumesababisha wanafunzi kujisomea kwa ufanisi zaidi.
Wahitimu hao wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Capri-point pia wameipa serikali kongole kwa kutatua changamoto ya uhaba wa walimu wa Sanaa na hivyo kuwezesha kurahisisha ujifunzaji kwenye masomo hayo.
Jumla ya wanafunzi Mia mbili wamehitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari Capri-Point










