Na Dawati la Habari Polisi Mwanza
Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na wadau wa uvuvi limefanikiwa kudhibiti uhalifu ukiwemo uharamia uliokuwa ukitendaka ndani ya ziwa viktoria kwa kufanya doria, misako na operesheni mbalimbali zilizofanikisha kukamata watuhumiwa , mali za wizi pamoja na zana haramu za uvuvi.
Mafanikio hayo yamebainishwa Oktoba 25, 2024 wilayani Busega mkoani Simiyu wakati wa kikao kazi cha Saba cha Makamanda wa Polisi mikoa ya kanda ya ziwa na wadau wa uvuvi kutoka mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Tarime Rorya, Kagera na Mara kwa lengo la kujadili usalama ndani ya ziwa viktoria.
Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa mikakati na maazimio ya kikao kilichopita, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafugwa amesema zaidi ya watuhumiwa 10,000 pamoja na zana haramu za uvuvi zikiwemo zaidi ya nyavu haramu 10,000 zilizokuwa zikitumika kuharibu mazao ya uvuvi zimekamatwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Kwa upande wake,Mkuu wa Operesheni maalum za Jeshi la Polisi Tanzania Naibu Kamishna wa Polisi DCP Mihayo Msekhela amesema kuwa "tangu tumeanza vikao hivi Kwa ukanda huu wa ziwa viktoria tumekuwa na mafanikio makubwa sana ya kudhibiti uhalifu ndani ya ziwa, oparesheni za Jeshi la Polisi ambazo ni shiriki zinazoshirikisha wadau wote zimekuwa na tija sana kwa kupunguza matukio ya uhalifu ukilinganisha na makosa yaliyoripotiwa mwaka 2021 wakati vikao hivi vilipoaanza"
DCP Msekhela ameongeza kuwa "awali kulikuwa kunaripotiwa makosa ya wizi wa boti, injini , wizi wa samaki na mauaji yalikuwa zaidi ya asilimia sabini ndani ya ziwa viktoria lakini leo hii ni injini kumi tuu ziliibiwa na watuhumiwa wamekamatwa wapo mahakamani hayo ni mafanikio makubwa sana".
Naye, Mkuu wa mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi amewataka wananchi wa kanda ya ziwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuzuia uhalifu ndani ya ziwa viktoria na maeneo ya nchi kavu kwa kutoa taarifa sahihi za uhalifu na wahalifu.
Kwa upande wa wananchi wameomba operesheni, misako na doria hizo ziendelee huku wakisisitiza ziwafikie wote hasa wanaotumia zana haramu za uvuvi na wanaopora mazao ya uvuvi kwa wavuvi.


.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)

.jpg)