Na Mwandishi Wetu
JUMLA ya wafugaji wadogo 92,831 na wadau wa mnyororo wa thamani wa maziwa wa Tanzania Bara na Visiwani-Zanzibar wamenufaika na Mradi Shirikishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa (TI3P) tangu ulipoanzishwa mwezi Machi mwaka 2022, ambapo asilimia 30 ya wanufaika hao ni wanawake.
Mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania - TADB pamoja na Bill & Melinda Gates Foundation huku ukitekelezwa kwa kushirikiana na Heifer International, Land O’Lakes Venture37 pamoja na Tanager.
Akizungumza wakati wa maonesho ya Wiki ya Maziwa Mkoani Iringa, Mratibu wa Mradi wa TI3P, Joseph Mabula, alisema mradi huo unalenga kutatua changamoto mbali mbali zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ndogo ya maziwa ili kuongeza uzalishaji, na kuboresha kipato cha wafugaji wadogo wa maziwa nchini.
Aliishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa uzito mkubwa sekta ndogo ya maziwa.
Mabula alisema tangu kuanza kwake, mradi umewezesha utolewaji wa mikopo wa zaidi ya shilingi bilioni 42 kwenye sekta ndogo ya maziwa ikiwalenga wasindikaji wa maziwa, wafugaji, wasambazaji wa pembejeo, pamoja na wadau wengine kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya maziwa.
Fedha hizo zimewezesha uanzishwaji wa viwanda vipya vya kuchakata maziwa pamoja na upanuzi na maboresho kwa jumla ya viwanda 17 vya usindikaji vimefikiwa kwa uwekezaji wenye thamani ya shilingi bilioni 22.8.
Aidha, alisema mradi umewezesha ununuzi wa mitamba 3,330 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 11.09, hatua iliyochangia kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya maziwa nchini.
Kupitia mradi huo, alisema wafugaji wameendelea kupata huduma za ugani, pembejeo bora, masoko, pamoja na huduma za kifedha kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ndogo ya maziwa, jumla ya wasindikaji 19 wa maziwa wamenufaika na programu za kuongeza uwezo, huduma za ugani, na ufanisi katika uzalishaji.
Katika kuhamasisha ushirikishwaji wa kijinsia na ukuaji jumuishi, alisema TADB ilitoa ruzuku linganifu yenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 kwa wafugaji wadogo 1,216, wakiwemo wanawake 397, ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa mitamba bora, uzalishaji, uchakataji na uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa maziwa.
Vilevile, biashara tano (5) zinazomilikiwa na wanawake zilipatiwa mitambo ya kuchemshia maziwa yenye thamani ya shilingi milioni 75 ili kuongeza fursa za masoko kwa wafugaji. Wasindikaji wanawake watano (5) walinufaika na ruzuku za TI3P, huku wasindikaji 12 wakipata ruzuku maalum za kuchochea usawa wa kijinsia katika biashara zao.
Katika kuboresha ukusanyaji na kuhakikisha ubora wa maziwa, alisema mradi umefanikiwa kuanzisha na kuimarisha vyama vya ushirikia/msingi 45 pamoja na vikundi mbalimbali vya wafugaji na wafanyabiashara kwenye seta ndogo ya maziwa.
Alisemaa vikundi hivyo kwa sasa vinakusanya zaidi ya lita 25,664 za maziwa kwa siku,hivyo kuchochea upatikanaji wa maziwa hususani kwa viwanda na wachakataji wadogo wa maziwa.
Mratibu wa Mradi huo, amesema kuwa mradi umefanikiwa kuanzisha vituo 23 vya ukusanyaji wa maziwa nchini kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 1.157 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo vyama vya ushirika, wafugaji, wasindikaji wa maziwa, na washirika katika utekelezaji wa mradi.
Mabula amehihimisha kwa kusema kuwa mradi huo unaendelea kushughulikia changamoto za kisera na kisheria zinazoathiri ukuaji wa sekta ndogo ya maziwa sambamba na kuzingatia masuala mtambuka kama usawa wa kijinsia na lishe bora kwa maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
Ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ndogo ya maziwa na kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa kupitia mradi wa TI3P pamoja na huduma za TADB.


Comments
Post a Comment