Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, amesema ameridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Manispaa ya Musoma kupitia Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Miji kwa Njia ya Ushindani Tanzania (TACTICS).
Amesisitiza juuu ya umuhimu wa miradi hiyo kukamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma zinazolengwa.
Mhandisi Mativila amesema hayo leo baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya mpango huo katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Katika ziara hiyo, alikagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara za Shaaban, Mkendo pamoja na Musoma Bus–Saa Nane, sambamba na miradi ya ujenzi wa jengo la ofisi, stendi ya mabasi ya Bweri na soko la Nyasho.
Akiwa kwenye ukaguzi huo, Mhandisi Mativila pia alishuhudia zoezi la upimaji wa tofali katika maabara maalumu kwa ajili ya kuhakiki ubora wa vifaa vinavyotumika kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, amesema kiwango cha ubora wa kazi kinachofanywa kinaridhisha na kinaendana na thamani ya fedha zinazowekezwa katika miradi hiyo ya maendeleo.
“Hadi sasa tumeridhishwa na utekelezaji wa miradi hii. Ubora wa kazi unaonekana na ni muhimu kuhakikisha viwango vinaendelea kuzingatiwa katika hatua zote za utekelezaji,” amesema Mhandisi Mativila.
Pamoja na pongezi hizo, amemtaka mkandarasi anayetekeleza miradi hiyo kuhakikisha anakamilisha kazi ndani ya muda uliokubaliwa kwenye mkataba ili miradi hiyo ianze kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati na kusaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Manispaa ya Musoma.
Amesema Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Miradi hiyo inayotekelezwa katika Manispaa ya Musoma ina thamani ya Shilingi bilioni 19.975 na inafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa TACTICS unaolenga kuboresha miundombinu ya miji na kuongeza ushindani wa kiuchumi pamoja na huduma za kijamii kwa wananchi.







Comments
Post a Comment