📍Wananchi waachwa wakilala nje kwenye baridi, mwekezaji adaiwa kugomea wito wa Mkuu wa Mkoa
Na Mwandishi Wetu, Muheza
KAMPUNI ya Amboni Plantation imewabomolea nyumba na kuwaacha wakilala nje kwenye baridi wananchi wa kaya 67, katika kitongoji cha Maisha Plus kilichopo kata ya Kigombe, wilayani Muheza mkoani Tanga.
Uharibifu huo wa dharura umefanyika Ijumaa iliyopita katika Kijiji cha Mshakangoto, ambapo kampuni hiyo inayolima mkonge imetumia uamuzi wa mahakama kuondoa familia hizo, ambazo nyingi ni za vibarua na wastaafu wa shamba hilo.
Mbunge wa Muheza na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), alitembelea eneo hilo Leo Mei 26 kushuhudia uharibifu huo na kulaani kitendo hicho akikitaja kuwa ni unyama uliokosa utu.
Mhe. Mwinjuma alifichua kuwa, baada ya mwekezaji huyo kushinda kesi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batlida Burihan alimwita mwekezaji ili kuweka utaratibu wa kiungwana wa kuwahamisha wananchi lakini hakupatikana kwa simu zake zote za mkononi.
"Baada ya kuwa hapatikani kwenye simu, ndipo wamekuja kufanya unyama huu wa kujichukulia sheria mkononi. Hili ni jambo baya sana. Nakwenda kukutana na Mheshimiwa Rais kulisemea hili, nitamshawishi afute hati ya eneo hili ili tupate mwekezaji mwingine mwenye utu," alisema MwanaFA.
Msaada wa chakula na Ekari 37 watamilikishwa
Ili kunusuru wananchi hao wasife kwa ugonjwa wa nimonia kutokana na mvua za mchoo zinazoendelea, Mbunge huyo amekabidhi msaada wa dharura wa tani mbili za chakula na fedha taslimu wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 12,160.
Msaada huo unahusisha kilo 1,000 za mchele, kilo 1,000 za sembe, kilo 200 za maharage, kilo 200 za sukari, lita 40 za mafuta ya kupikia, chumvi ya Sh. 60,000, pamoja na kupewa fedha taslimu Shilingi 100,000 kwa kila kaya.
Msaada huo wa mbunge ametoa kwa kushirikiana na Mwenyekti wa CCM wa mkoa Ustadh Rajab Abdurahaman.
MwanaFA aliongeza kuwa mwekezaji ametoa eneo jingine lililopo ndani ya shamba hilo lenye ekari 37 (ikilinganishwa na ekari 11.5 walizokuwa wakikaa), ambalo pia mwekezaji atasafisha, na wananchi hao watamilikishwa kwa hati rasmi ili kuzuia migogoro ya baadae. Pia ameahidi kuweka mwanasheria wa kupitia upya hukumu hiyo ya mahakama.
Kilio cha Wananchi: "Walituvamia Tukiwa Kazini"
Wakizungumza kwa masikitiko, baadhi ya wananchi walieleza kuwa mwekezaji huyo alivamia saa tatu asubuhi wakiwa mashambani, akisindikizwa na mgambo waliotokea mjini ambao mbali na kubomoa waliiba mali zao.
"Wamebomoa nyumba yangu, mifugo imekufa na wale mgambo wameiba fedha zangu na chakula vyote. Huu ni uonevu mkubwa," alilalamika mwananchi Jane Sekela.
Naye Meneja wa zamani wa shamba hilo tangu mwaka 1997, Venance Ndunga, alisema kihistoria eneo hilo tangu enzi za kampuni ya kwanza ya Amboni Properties lilitengwa kitalamu kama 'Reserve Labour Camp Area' kwa ajili ya kambi ya wafanyakazi wanaostaafu (Manamba) ili wajenge nyumba zao za kudumu, na halipo ndani ya ramani ya shamba la mwekezaji ya mwaka 2010.
Diwani wa Kata ya Kigombe, Shahongwe Mgandi, amewasihi wananchi hao kuendelea kuwa wavumilivu na kutoingia mitaani kufanya fujo, akihakikisha kuwa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) viko kazini usiku na mchana kupata suluhu ya kudumu ya makazi yao.





















Comments
Post a Comment