Na Mwandishi Wetu, Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, ameunda Kamati Maalum ya dharura kuchunguza sakata la uvunjaji wa nyumba za wananchi Kijiji cha Msakangoto kilichopo kata Kigombe wilayani Muheza.
Uamuzi huo umekuja kufuatia msukumo mkubwa wa kisiasa na kibinadamu uliowekwa na Mbunge wa Muheza na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), ambaye aliahirisha majukumu ya kitaifa na kupiga kambi kijijini hapo kushughulikia dharura hiyo.
MwanaFA, ambaye alifika katika Kitongoji cha Maisha Plus Mei 26 na kurejea Mei 28, alionyesha kukerwa na kitendo cha Kampuni ya Amboni Plantation kubomoa nyumba za kaya 67 kienyeji na kuwaacha wananchi wakilala nje, hatua iliyomfanya amfuate RC ofisini kwake na kuweka mikakati ya kuwajibisha waliohusika.
Ubomoaji wa Siri Bila Polisi Kujua
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Juni 1, 2026, Balozi Batilda amesema Serikali inahitaji ufafanuzi wa kina kuhusu mchakato huo, baada ya kubainika kuwa oparesheni hiyo ilifanyika Mei 22, 2026, kwa siri bila ushirikishwaji wa Jeshi la Polisi wala viongozi wa Wilaya na Mkoa.
Amesema kamati hiyo itachunguza sababu za kutoshirikishwa kwa mamlaka husika, na kutathmini kama kulikuwa na maandalizi yoyote ya kibinadamu ya kuwapa wananchi hao makazi mbadala na huduma muhimu za kijamii kabla ya kuwashushia tingatinga.
"Hatupingi amri halali ya mahakama, lakini tunataka kujua utaratibu uliotumika, maandalizi yaliyofanyika na namna wananchi hawa watakavyoendelea na maisha yao katika maeneo mapya. Huwezi kufanya oparesheni kubwa namna hii bila vyombo vya ulinzi na usalama kujua," alisisitiza Balozi Batilda.
Siku Tano za Kiama na Uchunguzi wa Ekari 37
Mkuu huyo wa Mkoa alibainisha kuwa kamati hiyo imepewa siku tano tu, kuanzia leo Juni 1 hadi Juni 5, 2026, kukamilisha uchunguzi huo na kuwasilisha taarifa rasmi kwa Serikali ya Mkoa ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wakiukaji wa taratibu.
Miongoni mwa mambo yatakayochunguzwa kitalamu ni ubora wa eneo jipya la ekari 37 lililotengwa na mwekezaji ambalo wananchi wamelitolea mashaka kuwa ni mkondo wa maji, pamoja na athari za kisaikolojia na kielimu kwa watoto wanaosoma shule za jirani.
Balozi Batilda alitoa onyo kali kwa taasisi au mtu yeyote atakayethubutu kutekeleza amri za uhamishaji bila kushirikisha vyombo vya dharura vya dola, akisema ushirikishwaji ni nguzo kuu ya kulinda amani na utu wa Watanzania.
Wakati suluhu ya kudumu ya fidia na makazi ikisukumiwa mbele, Serikali ya Mkoa imechukua hatua za dharura kuwapatia wahanga hao maturubai makubwa na mahema ili kujikinga dhidi ya baridi na mvua zinazoendelea kunyesha.










Comments
Post a Comment