Skip to main content

@marato_tv

@marato_tv
#sauti_ya_jamii

NAIBU WAZIRI MWINJUMA ARIDHISHWA NA UFUNGAJI VITI MKWAKWANI


 Serikali itaendelea kuboresha viwanja mbalimbali vya michezo nchini ili viweze kutumika katika michuano ya kimataifa hata baada ya Mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2027 (AFCON 2027).

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, mara baada ya kutembelea na kukagua usimikaji wa Viti katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga leo Juni 5, 2026.





Mhe. Mwinjuma ameupongeza Uongozi wa uwanja huo chini ya Meneja Nassoro Makau, kwa kufanya ubunifu mkubwa wa kuvipanga vizuri viti kwa rangi, ikiwa ni viti vilivyotolewa na Serikali katika uwanja wa Benjamin Mkapa, hatua inayoupendezesha uwanja huo wa kihistoria.

Amesema, uboreshaji wa viwanja vya michezo nchini ni sehemu ya maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye Serikali yake ya Awamu ya Sita imewekeza kwa kiwango cha hali ya juu katika ukarabati wa viwanja kama Uhuru na Mkapa, pamoja na ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa Arusha.

"Zoezi la usimikaji wa viti hapa Mkwakwani limefanyika kwa ukamilifu mkubwa. Serikali kwa kushirikiana na wadau itaona namna ya kukamilisha sehemu iliyobaki kadiri rasilimali zitakavyopatikana. Nawaomba wananchi na wapenda michezo kutunza miundombinu hii na kuepuka uharibifu ili viwanja vyetu viwe endelevu," amesisitiza Mwinjuma.

Ametoa wito kwa sekta binafsi na wadau mbalimbali wa soka nchini kujitokeza kushirikiana na Serikali ili kuweka nguvu ya pamoja katika kukamilisha maeneo madogo yaliyobaki uwanjani hapo ili kuendana na kasi ya soko la soka la kisasa duniani.

Akiwasilisha taarifa ya ukarabati huo, Meneja wa Uwanja wa CCM Mkwakwani, Nassoro Makau, alisema kuwa katika awamu ya kwanza, Serikali iliwaletea jumla ya viti 6,500 ambavyo vimeshafungwa kikamilifu, huku kukiwa na upungufu wa viti 2,500 ili kukamilisha maeneo yote.

Makau alifafanua kitalamu kuwa viti hivyo vimeshafungwa kwenye Jukwaa Kuu (Main Stand), jukwaa la Reli Moja na Reli Mbili, huku jukwaa maarufu la "Urusi" likiwa ndilo eneo pekee lililobaki ambalo halijafungwa viti kwa sasa. Baada ya ukarabati huu, uwezo wa uwanja huo sasa utakuwa ni kubeba watazamaji 9,000 waliokaa kwenye viti.





Comments