MADIWANI wa Manispaa ya Kibaha wameeleza kuwa ziara yao ya mafunzo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Mji Tunduma italeta manufaa makubwa katika kuongeza mapato na kuimarisha miradi ya maendeleo ya Manispaa hiyo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas amesema madiwani pamoja na wataalamu wa halmashauri wamepata uzoefu mkubwa kuhusu usimamizi wa mapato na uendeshaji wa vitega uchumi vinavyochangia maendeleo ya wananchi.
Amesema katika Jiji la Mbeya wamejifunza namna miradi ya ujenzi wa maduka, ukumbi pamoja na maeneo ya mapumziko inavyoongeza mapato ya halmashauri na kutoa huduma bora kwa wananchi na wafanyabiashara.
Kwa upande wa Halmashauri ya Mji Tunduma, Dkt. Nicas amesema wamevutiwa na mfumo wa parking za malori unaochangia mapato makubwa ya Halmashauri hiyo kutokana na shughuli za biashara mpakani mwa Tanzania na Zambia.
“Tumepata mambo mengi ya kujifunza. Tumeona namna parking za malori zinavyoongeza mapato Tunduma, pamoja na usimamizi wa maduka ya halmashauri yaliyopo mpakani. Haya yote yataisaidia Manispaa ya Kibaha kuongeza mapato na kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema Dkt. Nicas.
Ameongeza kuwa Manispaa ya Kibaha ipo katika mpango wa kujenga parking ya malori pamoja na kuendeleza vitega uchumi mbalimbali ili kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri.
Meya huyo pia amemshukuru na kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha kwa kuwezesha ziara hiyo ya mafunzo, akisema imewapa madiwani na wataalamu nafasi ya kujifunza mbinu bora za usimamizi wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo, madiwani na wataalamu walitembelea parking ya malori ya Halmashauri ya Mji Tunduma, maduka ya halmashauri yaliyopo mpakani mwa Tanzania na Zambia, pamoja na miradi mbalimbali ya vitega uchumi katika Jiji la Mbeya.





Comments
Post a Comment