RAIS wa Jamhuri ya Kenya, William Samoei Ruto, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania leo Mei 4, 2026, kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya Kenya na Tanzania.
Akiwa nchini, Rais Ruto atafanya mazungumzo ya ana kwa ana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kabla ya kuongoza mazungumzo rasmi yatakayojumuisha ujumbe wa nchi zote mbili.
Viongozi hao pia watazungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao hicho ambapo Mazungumzo hayo yanatarajiwa kujikita katika kuimarisha ushirikiano wa kindugu na kiuchumi, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, miundombinu na usafirishaji, pamoja na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa pande zote mbili.
Katika hatua nyingine muhimu, viongozi hao watashuhudia utiaji saini wa hati mbalimbali za makubaliano na mikataba ya ushirikiano, sambamba na kushiriki Jukwaa la Biashara litakalowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania na Kenya.
Kesho, Mei 5, 2026, Rais Ruto anatarajiwa kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, kabla ya kuhitimisha ziara yake na kurejea Kenya baadaye siku hiyo.
Ziara hii inatazamwa kama hatua muhimu ya kuimarisha zaidi mahusiano ya kihistoria na ya kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili ya Afrika Mashariki.

Comments
Post a Comment