Na Ghati Msamba; Serengeti
MKURUGENZI wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania Tanzania, Dk. Rhimo Nyansaho, ametoa mchango wa Shilingi Milioni 20 kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ring’wani kilichopo katika Kata ya Ring’wani, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara.
Dk. Nyansaho alikabidhi mchango huo kupitia Mwakilishi wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco, katika harambee iliyofanyika Desemba 23, 2024, Kijijini Ring’wani. Harambee hiyo ilihusisha wananchi, wadau wa maendeleo, na viongozi wa serikali.
Katika harambee hiyo, zaidi ya Shilingi Milioni 84 zilikusanywa, ambapo Dk. Nyansaho alitoa Shilingi Milioni 20 taslimu. Serikali ilitoa ahadi ya Shilingi Milioni 50, na fedha nyingine zilizopatikana ni Shilingi Milioni 6.3 na Shilingi Milioni 8.2 zilizochangwa na Umoja wa Maendeleo wa Ring’wani, na ziliwekwa kwenye akaunti ya ujenzi wa Zahanati hiyo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti Angelina Lubella alieleza kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na Zahanati, na aliipongeza Umoja wa Maendeleo wa Ring’wani kwa juhudi zao za kuchangia na kuhamasisha jamii ili kuhakikisha Zahanati inajengwa.
Serikali itatoa Shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Zahanati hiyo, ambapo fedha hizo zinapaswa kutumika vizuri ili kumaliza ujenzi ifikapo Machi 2025.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayubu Makuruma, alisisitiza kuwa ujenzi wa Zahanati hiyo ni muhimu kwa huduma za afya kwa wananchi. Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Serengeti, Mrobanda Japan Mkome, aliwahimiza wasomi kujenga utamaduni wa kusaidia jamii kupitia elimu, ujuzi, na vipato vyao, badala ya kuwa na tabia ya ubinafsi. Alieleza kuwa kusaidia jamii ni baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Dk. Genchwere Makenge, akielezea kuhusu ujenzi wa Zahanati hiyo, alisema kuwa Kijiji cha Ring’wani kina wakazi 2,727, wakiwemo wanawake 1,388 na wanaume 1,339. Ujenzi wa Zahanati ulianza mwaka 2015 kwa kujenga msingi, na baadaye boma lilijengwa mwaka 2016-2017 chini ya uongozi wa Kijiji. Gharama za kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo zinakadiriwa kuwa Shilingi Milioni 100, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la OPD, choo cha wagonjwa, na kichomeo cha taka.
Dk. Makenge alieleza kuwa kukosekana kwa Zahanati katika kijiji hicho kumekuwa kikiwasababishia wanawake kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za afya katika vijiji vya Kemugesi na Kenyana, na kusababisha changamoto kubwa hasa kwa wajawazito na watoto wanaohitaji chanjo.
Edina James, mkazi wa Kijiji cha Ring’wani, alieleza kuwa wananchi wa kijiji hicho wanashauku kubwa ya kupata huduma za afya karibu na makazi yao, na kwamba kukamilika kwa Zahanati hiyo kutakuwa mwarobaini wa kutatua changamoto ya kutembea umbali mrefu ili kupata huduma za afya.