KATIKA kuendeleza mshikamano wa kijamii na kuunga mkono juhudi za maendeleo ya kiroho, Mbunge wa Jimbo la Kivule, Ojambi Massaburi, kupitia Katibu wake Wakili Msomi Mashaka Nyadhi, ameongoza harambee ya uchangiaji kwa ajili ya ununuzi wa eneo la Kanisa la E.A.G.T Lango la Rehema, lililopo Mtaa wa Magole A, Kata ya Kivule, Mei 3, 2026.
Harambee hiyo imekuwa na mafanikio makubwa baada ya kufanikisha kukusanya jumla ya shilingi 8,448,000, fedha zitakazosaidia kutimiza azma ya kanisa hilo kupata eneo lake rasmi na kuimarisha huduma za kiroho kwa waumini.
Akihutubia waumini na wananchi waliojitokeza kushiriki tukio hilo, Nyadhi aligusia nguvu ya umoja na umuhimu wa kujitolea kwa maendeleo ya jamii.
“Ushirikiano wetu ndio msingi wa mafanikio ya kweli. Tunapoweka nguvu pamoja, hakuna linaloshindikana ,haya ndiyo maendeleo tunayoyahitaji katika jamii yetu,” alisisitiza.
Aidha, aliwahamasisha kuendeleza moyo wa kuchangia na kushirikiana, akibainisha kuwa uwekezaji katika taasisi za kijamii na kiroho ni sehemu muhimu ya kujenga jamii imara na yenye maadili.
Katika hafla hiyo, Nyadhi aliambatana na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Magole A, Athuman Muhogo, ambaye aliwasilisha salamu za Diwani wa Kata ya Kivule, CPA Rajabu Manyinya, akithibitisha uungwaji mkono wa viongozi wa eneo hilo katika jitihada hizo za maendeleo.
Harambee hiyo imeacha alama ya mshikamano, ikidhihirisha kuwa pale jamii inapoungana kwa lengo moja, mafanikio huwa ni ya uhakika.








Comments
Post a Comment