
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, leo Mei 4, 2026, akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo, amesema Serikali imejipanga kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya teknolojia duniani.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo leo Mei 4,2026, Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Poul Makonda amesema Kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa, Serikali imeanzisha Kongoo ya Kiswahili ya Taifa (KOKITA), mradi mkubwa unaolenga kukusanya na kuhifadhi msamiati wa Kiswahili kwa matumizi ya kidijitali.
“Tunataka Kiswahili kisiwe nyuma katika mapinduzi ya teknolojia; KOKITA ni daraja la kukipeleka katika matumizi ya Akili Unde (AI),” amesema Makonda.
Ameeleza kuwa kuanzia Julai 2025 hadi Aprili 2026, jumla ya maneno milioni 22 yameingizwa kwenye kongoo hiyo, na kufikisha maneno milioni 61, huku lengo likiwa kufikia maneno milioni 100.
Aidha, ushirikiano unaendelea kuimarishwa na taasisi kama Mozilla Foundation ili kuongeza uwepo wa Kiswahili katika teknolojia.
Katika hatua ya kimataifa, Makonda amesema Kiswahili kimeandika historia baada ya kukubalika kuwa lugha rasmi ya UNESCO mwaka 2025.
“Hii ni hatua kubwa kwa Afrika; Kiswahili sasa kinazungumza na dunia kwa sauti rasmi zaidi,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa Kiswahili sasa ni lugha rasmi katika jumuiya mbalimbali za kikanda na kimataifa, huku likiwa pia na siku yake maalum ya maadhimisho kila Julai 7.
Wizara pia imeanza mazungumzo na kampuni kubwa za teknolojia kama Meta Platforms, TikTok na Google ili kupanua matumizi ya Kiswahili kwenye majukwaa ya kidijitali.
“Lengo ni kuongeza ajira na kipato kwa vijana kupitia maudhui ya Kiswahili mtandaoni,” amesema Makonda.
Kuhusu michezo, amesema Serikali imeanza usanifishaji wa istilahi 420 za michezo ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya Africa Cup of Nations 2027.
Katika kulinda lugha na utamaduni, BAKITA imerusha vipindi 1,057 kupitia redio na televisheni pamoja na kutoa mafunzo ya Kiswahili fasaha kwa watumishi mbalimbali.
“Asiyefahamu lugha, hafahamu mila; tunalinda Kiswahili kwa vitendo,” amesema.
Aidha, Kongamano la tano la idhaa zinazotangaza kwa Kiswahili duniani lilifanyika jijini Arusha katika ukumbi wa AICC, likilenga kuimarisha mchango wa vyombo vya habari katika kukuza lugha hiyo.
Kwa sasa Tanzania ina vituo 55 vya kufundisha Kiswahili kwa wageni, hatua inayozidi kuifanya lugha hiyo kuenea kimataifa.
Katika upande wa historia, Serikali inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, kwenye eneo la ekari 424.6.
Makonda amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mradi huo, akisema, “Tanzania itaendelea kuwa kitovu cha kumbukumbu za ukombozi wa Afrika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”


Comments
Post a Comment