Kamanda Brigedi ya Faru Brigedia Jenerali Gabriel Elias Kwiligwa amewataka wataalam wa Zimamoto na Uokoaji wa JWTZ kuwa wazalendo kwa kuutumia ujuzi walionao kwa manufaa ya Jeshi na Taifa kwa ujumla .
Brigedia Jenerali Kwiligwa ameyasema hayo wakati akifunga kikao kazi cha wataalam wa Zimamoto na uokoaji wa JWTZ kilichofanyika katika ukumbi wa Kikosi cha Usafirishaji Mwanza (MTC) tarehe 27 Machi 2026.
Ameainisha kuwa kufuatia kukua kwa sayansi na teknolojia majanga ya asili na yale yanayotokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu yameongezeka hivyo ni muhimu kwa wataalamu hao kuwa tayari muda wote wanapohitajika kutoa msaada.
Aidha, amesisitiza kuwa Makao Makuu ya Jeshi yataendelea kutoa kipaumbele kwa wataalam wa Zimamoto na Uokoaji katika kuwapatia Mafunzo na vitendea kazi ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kukabiliana na Majanga Kanali Juma Emmanuel Katunge amesema kuwa kikao hicho kimekuwa na tija kwa wataalam hao kwani wamebadilishana uzoefu na kuondoka wakiwa na uelewa na utayari wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao.
Kikao kazi cha wataalam wa Zimamoto na uokoaji wa JWTZ kimefanyika kuanzia tarehe 23 hadi 27 Machi 2026.




