Na Mashaka Mhando, Tanga
SHIRIKA la Tanga Yetu Initiative imeanza kutekeleza miradi mbalimbali kwa vijana yenye lengo la kuwainua kiuchumi kupitia elimu, uvuvi, mazingira na teklonojia ya Mawasiliano ya Habari.
Akizungumza wakati wakizindua miradi hiyo ya awamu ya pili, Mratibu wa miradi wa Tanga Yetu, Patrick Waziri alisema progamu hiyo itayodumu kwa miezi 21 inatekelezwa kwa mwamvuli wa miradi ya majiji inayofadhiliwa na shirika la nchini Uswisi la Botnar Foundation.
Alisema lengo la kutekeleza miradi hiyo ni kuendeleza afya na ustawi wa watoto na vijana wa Jiji la Tanga ili kuwainua kiuchumi.
Alisema awali walitekeleza miradi ya awamu ya kwanza iliyoanza mwaka 2019 nakuishia 2023 ambayo walitekeleza miradi 20 ikiwemo kufanya utafiti uliozaa kupanuka kwa wigo na kuongeza miradi zaidi.
"Leo tunazindua miradi ya elimu, mazingira kwa maana suala la ukusanyaji wa taka, uchumi wa blue kwa kufanya kilimo Cha kisasa kupitia bahari na vijana kufundishwa masuala la teklonojia," alisema Waziri.
Alisema katika uchumi wa blue watawafundisha vijana namna kulima zao la mwani na kupata masoko yake, ufugaji wa kaa, majongoo bahari na kamba kochi.
Akifafanua zaidi mmoja ya waelimishaji katika suala la elimu Godfry Telli alisema watajikita zaidi katika kuwafundisha walimu 60 walimu wawili kutoka katika shule 30 ili waweze kuboresha ufundishaji na watoto wajue Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.
"Awamu ya kwanza tulipita shule 10 tukakuta wanafunzi 3,800 wa darasa la tatu hadi la sita hawajui Kusoma, Kuandika na Kuhesabu hivyo tunataka kukuza ubora wa elimu katika Jiji la Tanga," alisema.
Naye msimamizi wa ufundishaji katika uchumi wa blue Omari Mohamed alisema kuwa watajikita zaidi kufanyia kazi changamoto ambazo zilijitokeza katika awamu ya kwanza ikiwemo ufugaji wa Kaa ambao watawaweka katika maeneo ya kisasa ili wasife kabla ya kuuzwa.
Alisema wakulima wa zao la Mwani wataunganishwa katika kituo kimoja ambacho hicho kitahusika kutafuta masoko ya kuuzwa ndani na nje ya nchi baada ya kupatikana masoko nchi za Ulaya.
Kuhusu suala vijana kufundishwa teklonojia msimamizi wa teklonojia hiyo kutoka Swahili Digital Yelsant Mlaseko alisema vijana 250 wa Jiji la Tanga watapatiwa mafunzo hayo.
Suala la mazingira msimamizi wa mradi huo Frank Kalongole alisema wataanza na kata tano za Jiji la Tanga na watakuwa na waokotaji kata 400 ambazo zitawekwa katika kituo kimoja.
Awali akizindua mpango huo Meya wa Jiji la Tanga Abrahaman Shilow alilipongeza shirika la Tanga Yetu kwa kuja na mpango huo ambao utasaidia kuwainua vijana wa Tanga kiuchumi.
Hata hivyo, alisema pamoja na Utekelezaji wa mpango huo pia shirika hilo likae na vijana kujua ndoto zao za baadae na kuwasilisha taarifa ambazo zitachakatwa ili kuwawezesha kiuchumi.




Comments
Post a Comment