Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amepokea tuzo maalum kutoka kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, kwa mchango wake mkubwa katika utekelezaji wa afua za lishe kwenye sekta mtambuka. Tuzo hiyo ilikabidhiwa hivi karibuni wakati wa hafla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe uliofanyika kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort, Jijini Mwanza. Tuzo hii ni ishara ya kutambua juhudi za Mhe. Mtaka na Mkoa wa Njombe katika kuboresha hali ya lishe miongoni mwa wananchi.
Akizungumza Ofisini kwake, Mhe. Anthony Mtaka alieleza kufurahia kutambuliwa kwa mchango wa Mkoa wa Njombe kwenye sekta ya Lishe. "Tuzo hii ni uthibitisho kwamba jitihada zetu za kupambana na udumavu na kuboresha afya na lishe katika Mkoa wetu zinaonekana. Hatuishii hapa, Njombe itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha tunatokomeza udumavu kupitia mipango madhubuti ya lishe," alisema Mhe. Mtaka alipokuwa akiongea na Afisa Habari Msaidizi, Bw. Chrispin Kalinga.
Mhe. Mtaka alisisitiza kuwa Mkoa wa Njombe utaendelea na mikakati mbalimbali ya kuimarisha lishe kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kupitia kampeni ya Lishe yenye jina Lishe ya Mwanao, Mafanikio yake na kuzingatia kaulimbiu inayosema: "Kujaza Tumbo sio Lishe, Jali Unachomlisha." Aliongeza kuwa dhamira yao ni kuhakikisha kila mwananchi anapata lishe bora, ambayo ni msingi wa maendeleo endelevu. Mkoa wa Njombe umedhamiria kuondoa kabisa tatizo la udumavu kupitia kampeni na afua zinazolenga kuboresha lishe katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.




Comments
Post a Comment