Wakati mashindano ya mkuu wa majeshi Generali John Jacob Mkunda, yakitarajia kuanza Aug.19 mwaka vikundi mbalimbali vya utamaduni na muziki wa dansi vimeanza kujifua vikali huku kila mmoja akijinasibu kuondoka na ushindi katika mashindano hayo.
Mashindano hayo ya kwanza nchini yanatarajia kufanyika kwenye ukumbi wa jeshi wa Msasani Beach Club yanalenga kuhuisha tamaduni na muziki wa dansi ambao umeanza kutoweka kwa miaka ya hivi karibuni.
Katika mashindano hayo yanayotarajiwa kufunguliwa ma waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Damasi Ndumbaro, yatahusisha vikundi kumi vya muziki wa Dansi na tisa vikiwa vikundi vya ngoma za asili.
Waandishi wa habari wakiwa katika maeneo ya chuo cha mafunzo ya muziki na Sanaa cha jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania eneo la Mwenge,wameshuhudia kikundi cha utamaduni cha ngoma cha Mwenge Cultural kikijifua vikali kwa huku nyimbo na tambo mbalimbali zikisikika hali inayoashiria maandalizi mazuri kuelekea mashindano hayo.
Nako kwenye muziki wa dansi kikundi cha Mwenge Jazz wana Paselepa wakiendelea na mazoezi makali huku wakishusha vibao vyao vikali vilivyowahi kutamba miaka ya zamani.
Kiongozi wa bendi hiyo Salum Dialo akaeleza walivyojipanga kuelekea mashindano hayo ya mkuu wa Majeshi ambapo wamesema wao kama walimu wanakwenda kuyatumia mashindano hayo kama sehemu ya kuwafundisha washindani wao namna ya kupigia ala za muziki uhodari na tambo zao katika kusakata muziki.
Kwa upande wake kikundi cha ngoma za utamaduni, Mbweni Cultural Group pamoja na kikundi cha muziki wa dansi Mbweni Jazz almaarufu wazee wa Jodari wameonesha mbwembwe za kufa mtu huku wakisema kuelekea mashindano hayo, wamewatahadharisha wapinzani wao kuwa kutokana na maandalizi waliyoyafanya kuwa hawatofanya mzaha hata kidogo na kwamba wamejipanga vyema kuhakikisha wanaibuka washindi kutokana na mazoezi makali wanayoyapata kupitia viongozi wao.
Wamesema kupitia mazoezi hayo wanayofanya kuanzia asubuhi mpaka usiku ni wazi kuwa hawatokua na msamaha kwa yeyote watakaeenda kukutana nae katika mashindano hayo kwani wao watahakikisha wanalinda heshima waliyojijengea tangu awali katika utoaji burudan katika vikundi vya majeshi.
Katika upande wa muziki wa dansi wazee hao wa Jodari wameeleza walivyojiandaa huku wakionesha tambo na majigambo katika muziki wanapiga kando ya fukwe za bahari ya hindi.




.jpg)




Comments
Post a Comment