Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amewataka wanachama wanaokusudia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho kujipima kwanza na kuhakikisha wana uwezo wa kutekeleza majukumu ya nafasi wanazoziomba.
Wasira ametoa kauli hiyo leo, Novemba 6, 2026, jijini Arusha, wakati akizungumza na wanachama wa CCM, akisisitiza kuwa uongozi unapaswa kutokana na ridhaa ya wanachama na si uwezo wa kifedha wa mgombea.
Amesema CCM ilianzishwa kwa dhamira ya kutetea wananchi wa kawaida na kupambana na dhuluma, hivyo chama hicho hakipaswi kushuhudia dhuluma bila kuchukua hatua, akieleza kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na misingi ya chama.
Amesisitiza kuwa wanachama wana wajibu wa kuwachagua viongozi wenye uwezo na wanaoielewa vizuri misingi ya CCM, akifananisha uongozi na udereva ambapo mtu asiyejua kuendesha gari hawezi kupewa jukumu la kuwa dereva bila kuhatarisha safari.
Aidha, amewataka wanaotaka kugombea nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya tawi, kata, wilaya, mkoa hadi taifa kujiuliza kama wana uwezo wa kuongoza, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu anayefaa kuendelea kuwa kiongozi milele.
Wasira amesisitiza kuwa mtu anayeamini hawezi kushinda uchaguzi bila kutumia fedha anapaswa kuachana na kugombea, akitaka viongozi wachaguliwe kwa hiari na ridhaa ya wanachama.










Comments
Post a Comment